Saturday, December 2, 2017

Mawingu Tz

Arsenal,Man United Kuuana Leo Apo Emirates…Ni Vita Ya Fomesheni..Nani Kupaki BUS Leo?


Vita ya fomesheni huko Emirates usiku wa leo Jumamosi. Mwenyeji Arsene Wenger ataingia na 3-4-3; golini Petr Cech na mabeki wake watatu wa kati ni Nacho Monreal, Shkodran Mustafi na Laurent Koscielny huku kwenye safu kiungo, wing-back kulia ni Hector Bellerin, kushoto ni Sead Kolasinac wakati viungo wa kati ni Granit Xhaka na Aaron Ramsey, huku safu ya ushambuliaji watatu kutakuwa na Alexis Sanchez kushoto, Olivier Giroud katikati na Mesut Ozil kulia.
Mgeni, Jose Mourinho yeye atakuwa na fomesheni yake ya 4-2-3-1, huku kukiwa na mabadiliko kwenye sehemu ya kiungo ya kati baada ya Nemanja Matic kuwa na hatihati.
Mourinho anafahamu wazi namna bora kabisa ya kuidhibiti Arsenal basi ni kumnyima mipira Ozil, huku Wenger akifahamu wazi ana kazi ya kumdhibiti Paul Pogba, Marcus Rashford na Anthony Martial, walio hatari zaidi.
Mchezaji mwingine tishio wa Arsenal ni Kolasinac, lakini kwa bahati mbaya kwenye upande wake kutakuwa na Ashley Young, ambaye kwa sasa amekuwa fomu kweli kweli.
Rekodi zinaibeba Man United. Hii ni mechi yao ya 51 tangu iitwe Ligi Kuu na wababe hao wa Old Trafford wameshinda 22, sare 15 na Arsenal wameshinda mechi 13. Kiujumla kwenye ligi timu hizo zimekutana mara 196, Man United wakiongoza kwa kushinda mara 81.
Lakini,Man United hawajawahi kushinda Emirates tangu mwaka 2014, huku mara mbili za mwisho ilipokwenda kwenye uwanja huo ilichapwa 3-0 na 2-0. Leo kazi wanayo, wataibeba Arsenal kwa mbereko gani? Mechi hii pia ni vita ya Mourinho na Wenger.
Mara 17 walizokutana, Jose ameshinda nane, sare saba na Wenger ameshinda mbili tu. Kwa kifupi, Wenger hamuwezi Mourinho. Ufundi tu ndio utakaoamua matokeo ya mchezo huo.
Arsenal itahitaji kushinda ili kuendelea kutamba ndani ya Top Four, lakini Man United watataka kushinda pia ili kuzidi kuipa presha Manchester City kwenye mbio za ubingwa.
Man United imekuwa na ukuta mgumu zaidi msimu huu. Umeruhusu mabao manane tu katika mechi 14, wakati Arsenal wao wameruhusu mabao 16.
Man United pia imeizidi Arsenal kwa kufunga, yenyewe imefanya hivyo mara 32 wakati Arsenal imefunga mara 28.
Pengine hiki ni kipindi kizuri kwa Mourinho timu yake kupata matokeo kwenye mechi kubwa, kwani mechi saba alizocheza dhidi ya Top Six, ameambulia pointi tatu tu na bao moja.

Kazi sasa ni kwa Romelu Lukaku kubadili matokeo. Mourinho kuwadhibiti Arsenal ni kumweka kisiwani Ozil na Wenger kuwadhibiti Man United ni kumdhibiti Lukaku.
Fowadi huyo hafungi kwa siku za karibuni, lakini uwepo wake wa ndani ya uwanja umekuwa muhimu kwa kutoa nafasi kwa wengine kupachika wavuni. Sanchez bado hayupo kwenye ubora mkubwa na upande wake hii leo atakutana na Antonio Valencia.
Mechi nyingine za ligi hiyo, mabingwa watetezi Chelsea wao watakuwa nyumbani Stamford Bridge kuwakaribisha Newcastle, wakati Watford watakuwa wenyeji wa Tottenham huku Leicester City wakiwakaribisha Burnley.
Liverpool atakuwa na shughuli ya ugenini kwa Brighton huku West Brom wakiwa na kibarua mbele ya Crystal Palace na Stoke City wakiwa nyumbani kumenyana na Swansea City na Everton watacheza na Huddersfield.
Kesho Jumapili Bournemouth watakuwa nyumbani kucheza na Southampton huku vinara Man City watajimwaga Etihad kuwakaribisha choka mbaya, West Ham United.

Tupe Maoni Yako