Friday, December 8, 2017

Mawingu Tz

Mastraika wapya Yanga wategwa


KOCHA Mkuu wa Yanga, George Lwandamina, ameendelea kunoa vijana wake kwenye Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam, lakini ametamka jambo moja akionyesha kuwa safari hii hataki utani.
Unajua ametamka nini? Kocha huyo aliupa maagizo uongozi wa Yanga kumtafutia straika mmoja ama wawili wa kimataifa, huku mfukoni akiwa na jina la mmoja wao ambaye ni Bensua De Silva kutoka Guinea, huku jingine akipenyezewa na mabosi hao.
Jina la pili alilokuwa amepewa ni Badara Kella raia wa Sierra Leone ambaye kwa taarifa ambazo Mwanaspoti inazo ni kwamba atatua nchini Jumapili na Jumatatu De Silva naye atakuwa mazoezini.
Lakini Lwandamina, ambaye kwa sasa akili na nguvu zake anaelekeza zaidi katika kuhakikisha Yanga inafanya vema mechi za kimataifa na pia akipambana kutetea ubingwa wa Ligi Kuu Bara, amewachimba mkwara wageni hao kwamba wakijiona hawapo fiti wasije kabisa, kwa sababu hataki kupoteza muda.
Mzambia huyo baada ya kudokezwa kuwa wachezaji watatua nchini muda wowote kuanza wikiendi hii, aliwaambia mabosi wake kuwa wahakikishe mastraika hao wageni wanakuja wakiwa fiti kwani hataki kukosea tena.
“Nimeruhusu waje kwa ajili ya majaribio, lakini nataka wawe fiti kwani sitaki kupoteza muda mwingi kuwatazama. Nataka usajili wa awamu hii ufanyike kwa umakini,” alisema.
Kocha huyo aliyeifikisha Zesco United ya kwao Zambia nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2016, alisema mbali ya mastraika hao, mkononi mwake alikuwa na jina jingine la straika kutoka DR Congo, ila amempotezea.
“Kuna straika mwingine Mkongomani, ni mzuri lakini sihitaji kuwa na wachezaji wengi kutoka nchi moja, sipendelei kwenye timu yangu,” alifichua kocha huyo.
Washambuliaji waliopo Yanga kwa sasa ni Obrey Chirwa, Amissi Tambwe, Donald Ngoma ambao ni wageni, huku wazawa wakiwa ni Ibrahim Ajibu, Anthony Matteo na Emmnauel Martin.
PANGA LAZIMA
Ujio wa nyota hao wa kigeni na kusajiliwa kwa wachezaji wengine wawili mpaka sasa kwenye dirisha dogo akiwamo beki Mkongomani, Fiston Kayembe na straika Yohana Mkomola, huku wakimpigia hesabu Rashid Mohammed wa Prisons kutasababisha kutibuliwa kwa mambo kwa baadhi ya wazoefu Yanga.
Kusaini kwa Kayembe ili kuongeza nguvu katika safu ya ulinzi inafahamika kutaongeza nguvu katika nafasi ya beki ya kati ya Yanga iliyoruhusu mabao matano mpaka sasa katika Ligi Kuu Bara iliyosimama.
Lwandamina amekuwa akisisitiza kuwa wamemsajili Kayembe kwa ajili ya Ligi ya Mabingwa Afrika, hivyo ana nafasi kubwa ya kuanza kuonekana uwanjani mara tu baada ya Ligi Kuu Bara itakapoendelea.
Kayembe amerudisha ushindani katika beki ya kati, ambapo awali nahodha, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Abdallah Shaibu ‘Ninja’ na Andrew Vincent ‘Dante’
walikuwa wakichuana vikali kuwania nafasi ya kucheza sambamba na Kelvin Yondani, lakini sasa mambo yatakuwa tofauti.
Yondani pekee ndiye mwenye uhakika wa kuanza katika kikosi cha kwanza huku Cannavaro, Dante na Kayembe wakichuana kuwania nafasi nyingine moja. Hata hivyo Kayembe ndiye anayepewa nafasi kubwa ya kuanza licha ya kwamba ni mgeni.
Kwa upande wa ushambuliaji, Yanga izungumza na staa wa Prisons, Rashid aliyefunga mabao sita msimu wake wa kwanza wa kucheza Ligi Kuu Bara na ujio wake utamwondoa nyota mmoja wa kikosi cha kwanza.
Pia ujio wa kina De Silva kama mpango utatiki ni wazi utahitimisha maisha ya Amissi Tambwe na Donald Ngoma waliokuwa wakiandamwa na majeraha.
-Mwanaspoti

Tupe Maoni Yako