RASMI, Shirikisho la Soka nchini (TFF) limetangaza kusimamisha Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kwa wiki mbili kupisha michuano ya Kombe la CECAFA Challenge inayotarajiwa kuanza Desemba 3 hadi 17, mwaka huu nchini Kenya.
Ratiba mpya iliyotolewa na TFF inaonyesha sasa Desemba 22, 23, 24 na 26, zitakuwa siku za mechi za kuwania Kombe la Shirikisho la Azam yaani Azam Sports Federation Cup (ASFC).
Mechi zitakazochezwa katika siku hizo zitafahamika Desemba 5, mwaka huu ambako imepangwa droo ya timu 64 zitakazocheza Raundi ya Tatu ya ASFC.
Timu 64 maana yake ni kuwa timu 16 za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara; timu 24 za Ligi Daraja la Kwanza na timu 24 ambazo zimefuzu kutoka hatua awali; ya kwanza na pili.
Baada ya michezo hiyo, ratiba ya Ligi Kuu ya Vodacom itaendelea tena kwa michezo ya raundi ya 12 itakayofanyika Desemba 29, 30 na 31 kabla ya ligi kusimama tena kupisha michuano ya Kombe la Mapinduzi.
Michuano ya Kombe la Mapinduzi inatarajiwa kuanza Desemba 30 hadi Januari 13 mwakani visiwani Zanzibar.
Tupe Maoni Yako