Klabu ya Simba inatarajiwa kufanya mkutano wake kesho ambapo Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dk. Harrison Mwakyembe atakuwa mgeni mkutanoni hapo.
Mkutano huo mkuu wa wanachama unatarajiwa kufanyika kuanzia saa 4:00 asubuhi kwenye Ukumbi wa Mwalimu Nyerere, Dar es Salaam.
Ofisa Habari wa Simba, Haji Manara amesema kwamba wanataka kuutumia mkutano huo kumtangaza mshindi wa zabuni ya uwekezaji katika klabu yao.
Miezi miwili iliyopita klabu hiyo ilitangaza zabuni kwa wanachama wenye uwezo na mtaji kuanzia shilingi bilioni 20 kujitokeza na kufanya uwekezaji katika klabu hiyo katika mchakato wa mabadiliko ya muundo wa uendeshaji hadi kuwa wa hisa.
Alisema anaamini huo utakuwa ni mkutano wa kihistoria kwasababu wanakwenda kubadilisha muundo.
Awali, klabu hiyo ilisema mwekezaji atamiliki asilimia 50 ya hisa huku asilimia 10 zikitarajia kugawiwa kwa wanachama hai na nyingine 40 kuuzwa kwa wanachama.
Mfanyabiashara na mwanachama wa Simba, Mohamed Dewji ‘Mo’ aliwahi kuonyesha nia ya kuwekeza iwapo tu atapewa asilimia 50 ya hisa, ingawa hata hivyo, kesho itajulikana kama atakuwa yeye au wengine kutokana na vigezo vilivyokuwa vimewekwa.
Habari zaidi za simba-->Bofya Hapa
Tupe Maoni Yako