KOCHA mkuu wa Mtibwa Sugar, Zubery Katwila amezitaka klabu ambazo zinahitaji kusajili wachezaji kutoka kwake zikiwemo Simba na Yanga, zifanye haraka kwenda kufanya mazungumzo ili ajue jinsi ya kuziba nafasi kwa wale watakaoondoka.
Mtibwa Sugar ndio klabu pekee ambayo wachezaji wake wamekuwa wakigombewa mara kwa mara hasa na klabu kongwe za Simba na Yanga hivyo amewataka kama usajili huu wa dirisha dogo wana nia na wachezaji wake wafanye hima kwenda.
Akizungumza na Chandimu, Katwila alisema kuwa anasisitiza hilo kwasababu hatapenda kuona mchezaji wake anaondoka muda mfupi kabla ya dirisha la usajili kufungwa kwani haitampa nafasi ya yeye kutafuta mbadala.
“Binafsi sina mpango wa kusajili japo nasikia kwenye vyombo vya habari kuwa kuna wachezaji wangu wanahitajika na timu fulani hivyo nawaomba wale ambao wanawahitaji wachezaji wangu waje sasa hivi na si kusubiri muda umekwisha.“Kama ataondoka mchezaji yoyote basi nitatafuta mwingine wa kuziba nafasi yake ila jambo hili linapaswa kufanyika mapema, wanaowahitaji wachezaji wangu waje mapema ili nami niwe na nafasi ya kuziba nafasi, ” alisema Katwila
Upande wa Mwadui FC yenyewe imeelezwa kuwa ina mpango wa kusajili wachezaji wawili katika nafasi ya mshambuliaji na kiungo huku Kagera Sugar naye ikitaja kusajili wachezaji wawili pekee.
Mbeya City wao kuna majina yamependekezwa hasa nafasi ya kipa ambao ni David Kisu wa Njombe Mji na Hussein Sharif ‘Casillas’ kutoka Coastal Unione pamoja na nafasi ya beki namba mbili.
Tupe Maoni Yako