Thursday, December 28, 2017

Mawingu Tz

Yanga Sc Waiwangia Simba Mchana Kweupee


HUENDA kauli hii ikawa na ukakasi mkubwa kwa mashabiki wa Simba lakini ndiyo hivyo tena, kwamba wameambiwa na wenzao wa Yanga kuwa kama wanataka ubingwa wowote inabidi basi wasubiri msimu ujao wa 2018/19, kwani msimu huu hawana chao.
Yanga wamefikia kutamka maneno hayo mazito baada ya kuwaona watani zao hao wa jadi wakitupwa nje ya michuano ya Azam Sports Federation Cup (ASFC), wakikubali kichapo cha mabao 4-3 kutoka kwa Green Warriors kwa mikwaju ya penalti.
Simba ndio waliokuwa mabingwa watetezi wa michuano hiyo lakini wakajikuta wakipata aibu hiyo ya mwaka, kitendo kilichowafanya kuamua kumtimu kocha wao mkuu Joseph Omog na sasa wanahaha kutafuta mbadala wake.
Wakati Simba wao wakiangukia pua, watani zao hao wa jadi mwishoni mwa wiki iliyopita walijihakikishia kusonga mbele hatua inayofuata baada ya kuwashushia kipigo cha mabao 2-0, Reha FC ya Temeke mchezo uliochezwa Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam.
Kitendo hicho kimewafanya Yanga kukenua wakijiapiza kwamba msimu huu watakomba makombe yote na kama Simba wana hamu ya kunyakua ubingwa wowote, wanatakiwa kusubiri mpaka msimu ujao wa 2018/19 kwani msimu huu una wenyewe.
Msimu wa 2016/17, Yanga walifanikiwa kunyakua makombe yote, yani lile la Azam maarufu kama FA na la Ligi Kuu na sasa wanasema msimu huu tena watafanya hivyo kitu ambacho kinawafanya Simba kuweweseka hasa baada ya kuutema ubingwa wao wa FA.
Kitu pekee kinachoweza kuwabeba Simba kushiriki michuano ya kimataifa msimu ujao ni kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu msimu huu, lakini Yanga wamesema wanataka kutetea ubingwa wao, yaani wautwae mara ya nne mfululizo na kuvunja rekodi hiyo ikimaanisha Wekundu wa Msimbazi, wana mlima mrefu wa kupanda.
Baada ya mchezo dhidi ya Reha kumalizika, kocha msaidizi wa Yanga, Shadrack Nsajigwa, alisema malengo yao ni kuhakikisha msimu huu wanawafurahisha tena mashabiki wao kwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu na ule wa FA.
“Kwanza niwashukuru wachezaji wetu kwa jinsi walivyopambana mpaka kupata ushindi huu wa mabao 2-0, nadhani lengo letu ni kuhakikisha msimu huu tunafanya vizuri na kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu na hili Kombe la FA,” alisema Nsajigwa, kauli ambayo si nzuri kwa mashabiki wa Simba.
Mbali na kauli hiyo ya Nsajigwa, idadi kubwa ya mashabiki na wanachama wa kikosi hicho, wameshajihakikishia kwamba, Simba hawawezi kufanya lolote mbele ya timu yao.
“Simba kwishnei kabisa, yaani msimu huu watasubiri sana, wao kama wanataka ubingwa wasubiri msimu ujao wa 2018/19 kwani msimu huu Yanga tutaendelea kutesa, wameshatolewa kwenye kombe lao la FA, tena wakifungwa na timu ndogo sasa ndiyo Ligi Kuu wataweza,” walisikika wakisema mashabiki wa Yanga baada ya kushinda mchezo wao dhidi ya Reha FC.
Hata mitaani kwenye vijiwe mbalimbali mashabiki wa Yanga wanaamini Simba wamepoteza dira hasa kitendo cha kumtimua kocha wao mkuu, Joseph Omog, kinatajwa kwamba kutazidi kuwavuruga.
Yanga wanaamini watashinda michezo yao yote ya Ligi Kuu iliyobakia ikiwamo wa mwishoni mwa wiki hii dhidi ya Mbao FC, utakaochezwa Uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza, huku wakiamini Simba wataanza kupoteza dira dhidi ya Ndanda FC na kushuka kileleni.

Tupe Maoni Yako