Thursday, December 28, 2017

Mawingu Tz

Masoud Djuma Atoa Ya Moyoni Kuhusu Omog

Aliyekuwa kocha wa Simba Mcameroon, Joseph Omog.
KOCHA aliyeachiwa mikoba ya aliyekuwa kocha wa Simba Mcameroon, Joseph Omog, Mrundi Masoud Djuma, amesema kuwa anasikitishwa na kitendo cha kuona kocha huyo akiondoka huku wakiwa hawajamaliza jukumu lao la kuhakikisha wanaipa ubingwa klabu hiyo. Omog alifungashiwa virago vyake  wikiendi iliyopita baada ya kuiongoza Simba katika mechi  52 kati ya hizo ameshinda michezo 35, sare 11 na akifungwa michezo sita tu.

Championi Jumatano limepata nafasi ya kuzungumza na Masoud Djuma, lengo ni kujua muda mfupi atamisi nini kutoka kwa Omog ambaye wam e i s h i kwa muda mfupi.
CHAMPIONI: UTAKUMBUKA NINI KUTOKUWEPO KWA OMOG? DJUMA:
“Kama nimeishi na mtu vizuri kwa muda huu mfupi bila tatizo naye, nasikitika kumkosa maana nje na kazi tayari alikuwa akinichukulia mimi kama mtoto wake. “Wakati naanza kazi hapa Simba nilikuwa na matatizo yangu makubwa ambayo hakuna mtu mwingine yeyote niliyemueleza zaidi yake, lakini alinishauri kiasi kwamba niliona kama nipo nyumbani.

“Mbali na hivyo utaona ilifikia kipindi hata nikiwa na njaa nikitaka kununua hata mkate alikuwa ananizuia kulipa kama yupo karibu analipa yeye na anasema mimi ni mwanaye, hivyo sina haja ya kuhangaika mbele yake. “Kwa maana hii nasikitishwa sana na kuondoka kwake maana nitamisi mambo mengi kutoka kwake kwani kulikuwa kuna vitu namueleza yeye mwingine siwezi na alinivumilia sana.
Mrundi Masoud Djuma (katikati) akiongea na wanahabari.
CHAMPIONI: TAYARI UONGOZI UMEMTEMA JE, UTAWEZA KUENDELEZA USHINDANI UWANJANI BILA YEYE? DJUMA:
“Ameniachia jukumu kubwa sana na ukiangalia nina mechi kubwa na muhimu mbele yangu dhidi ya  Ndanda itakuwa ni moja ya mtihani wangu mgumu sana hivyo ninajipanga ili nisije kuanza kuleta kelele mpya.

“Timu ina presha kubwa kwa kila aliye mbele yetu kutokana na kuondoka kwa Omog ambaye naamini kuna waliomchukia na waliompenda hivyo kazi yangu sasa ni kuhakikisha nawaunganisha kuwa kitu kimoja.

“Hata mimi kuna wanaonipenda na wasionipenda hivyo jukumu langu sasa ni kupambana kadri ya uwezo wangu kuhakikisha nawaweka sawa ili huko mbele mambo yaweze kuwa mazuri tofauti na matarajio ya wanaotuombea mabaya.

CHAMPIONI: UMEJIFUNZA NINI KUTOKA KWA OMOG? DJUMA:
“Yapo mengi niliyojifunza kwake, la kwanza kubwa kuunganisha upendo ndani ya timu, pili wakati nakuja hapa pamoja na kwamba huko Rwanda nilikuwa kocha mkuu, baada ya kuitwa hapa Simba niliamua kuja kujifunza mambo mengi kutoka kwa Omog ambaye nilikuwa nikiamini kutokana na ukongwe wake hii fani.

“Lakini hata uzoefu wake kwenye ligi hii ya hapa Tanzania kwani amefundisha muda mrefu, kwa kuwa tayari niliamua kuja Simba na nikijua yupo yeye sikuangalia sana suala la madaraka ya ukocha mkuu zaidi ya kuangalia elimu niliyotarajia kuipata kutoka kwake.

“Jambo ambalo wengi walikuwa hawalifahamu maana kuna wale ambao walidhani mimi nipo hapa kutaka kuwa kocha mkuu tu na si kujifunza mengi ambayo nimeyapata kutoka kwake na kwamba nitammisi sana kwa sababu nilikuwa bado nahitaji elimu yake nzuri”.

CHAMPIONI: UNAWASHAURI NINI VIONGOZI JUU YA KUONDOKA KWA OMOG?
DJUMA: “Sina hata cha kushauri hapo kwani hata niseme nini ni ngumu kubadili hisia za wengi. Kwa wema alionifanyia mimi ningependa kuendelea kuwa naye tu lakini kwa kuwa kazi yetu hii ina changamoto kila ulipo maana siku zote timu ikifanya vizuri ni ya wote, ikifeli ya kocha.

“Ujue wakati nakuja kwa mara ya kwanza waandishi waliniuliza nimejipanga vipi na kutimuliwa hapa Simba, ila jibu langu siku hiyo niliwaambia kuwa kutokana na presha ya mpira inavyokuwa siku zote ukiwa kama kocha lazima ukiitwa sehemu unatakiwa kufungua begi lako nusu kwa muda wowote safari inaweza kukuta hivyo ili hata Omog alikuwa analijua vilevile kwangu linaweza kutokea muda wowote ule.

“Natambua changamoto nyingi sana kwenye mpira kwani utagundua kabla sijakuwa kocha mkuu huko Rwanda niliwahi kuwa kocha msaidizi kwenye timu ya vijana ya Burundi, hivyo nina uzoefu wa mambo mengi uwanjani na nje ya uwanja.

CHAMPIONI: UNAJISIKIAJE KUACHIWA SIMBA HUKU UKIWA KILELENI?
DJUMA: “Ninaona kama mtihani mkubwa sana kwangu kwani Simba ni timu kubwa na ina mashabiki wengi kupita wale wa Rayon, japo presha kwa watu wa mpira  huwa ni ileile.

“Simba wao wanahitaji ushindi kila siku na si kingine, kwa maana hiyo naona kama naingia kwenye mtego ila kwa kuwa Mungu ndiye kiongozi wa kila jambo hakika nitashinda tu kuanzia mechi iliyopo mbele yangu ili tuzendelee kuongoza ligi hii.”

“Mpira lazima uwe na ushirikiano kwa watu wote yaani kuanzia kocha, wachezaji na uongozi kwa ujumla kwani ili matokeo yapatikane baraka za kila mtu ndani ya timu ziweze kutumika hivyo mkiwa pamoja hata kutegemea kumtupia lawama kocha tu huwa kunapungua japo najua ipo siku moja hata mimi nitaondoka kwa kutupiwa mzigo huo kwani timu ikifanya vibaya ni ya kocha pekee.

Tupe Maoni Yako