Wednesday, December 20, 2017

Mawingu Tz

Yanga Kusajili Striker Huyu Hatari Kutoka Zanzibar Heroes


KITENDO cha Shirikisho la Soka nchini (TFF) kuongeza muda wa usajili wa dirisha dogo, ni kama kumewafaidisha Yanga ambao wanadaiwa kuanza kumnyemelea mmoja wa mastraika watatu wa timu ya taifa ya Zanzibar, Zanzibar Heroes.
Kurefushwa kwa muda huo wa usajili kunatokana na hitilafu zilizotokea siku ya mwisho ya usajili Desemba 15, mwaka huu baada ya kufeli kwa mtandao wa mfumo wa usajili (TMS), ambapo sasa timu zimeruhusiwa kusajili kwa wiki moja zaidi hadi Desemba 23.
Taarifa kutoka Yanga zinadai kuwa wanaweza wakatumia muda huo kusajili moja ya mastraika walioonyesha uwezo mkubwa wakiwa na kikosi cha Zanzibar Heroes, kilichomaliza katika nafasi ya pili ya michuano ya Kombe la Chalenji (Cecafa Senior Challenge Cup), iliyomalizika Machakos, nchini Kenya.
Kati ya mastraika hao, jicho zaidi lipo kwa Khamis Mussa Makame, anayeichezea Jang’ombe Boys ambaye alikuwa msaada mkubwa katika mchezo wa fainali dhidi ya Kenya, akifunga mabao mawili na mchezo huo kuamuliwa kwa mikwaju ya penalti, ambapo Zanzibar Heroes walifungwa 4-2.
Mbali na huyo, mwingine ni Ibrahim Hamad Ahmada, pamoja na Abdul Aziz Makame, pia wa Taifa Jang’ombe, ambaye naye aliuwasha moto kwenye michuano hiyo na sasa Yanga wanaangalia uwezekano wa kusajili mmoja kati ya hao.
Kigogo mmoja ndani ya Yanga ameliambia DIMBA Jumatano kwamba, wanafikiria kuongeza straika mmoja atakayeungana na akina Ibrahim Ajib, ambapo jicho lao wamelielekeza Zanzibar Heroes, kwani usajili wa wachezaji wa kigeni umejaa.
“Ni kweli tunaweza tukatumia nafasi hii kusajili mchezaji mmoja, inawezekana tukaangalia zaidi katika kikosi cha Zanzibar Heroes ambacho kilionyesha uwezo mkubwa kwenye michuano ya Cecafa.
“Tunafahamu kwamba TFF wamerefusha usajili huu ili kuwabeba Simba katika sakata lao la Asante Kwasi, lakini nasi ngoja tu tuangalie namna ya sisi kujiongeza wachezaji,” alisema.
Katika hatua nyingine kikosi hicho kimeendelea na mazoezi yao ya Gym na leo watakwenda katika Uwanja wa Uhuru kujifua wakijiandaa na mchezo wa Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) dhidi ya Rea.
Kocha Mkuu wa kikosi hicho, George Lwandamina, naye anatarajiwa kutua nchini leo Jumatano akitoka mapumzikoni kwao Zambia, baada ya Ligi Kuu kusimama kwa muda kupisha michuano ya Cecafa.

Tupe Maoni Yako