WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe, amewapa kazi washambuliaji, Shiza Kichuya na Ibrahim Ajib, kuhakikisha wanaendeleza makali katika michuano ya Chalenji ili kuipa ubingwa Kilimanjaro Stars.
Washambuliaji hao ni miongoni mwa wachezaji 23 wanaounda kikosi cha Tanzania Bara ‘Kilimanjaro Stars’, iliyoondoka jana jijini Dar es Salaam na Ndege ya Shirika la Kenya.
Kilimanjaro Stars itafungua dimba Jumapili kwa kucheza na timu ya Taifa ya Libya, ambao wanashiriki michuano hiyo kama mgeni mwalikwa.
Akizungumza katika hafla ya chakula cha usiku na kuaga timu hiyo iliyofanyika juzi kwenye Ukumbi wa Seascape, Mbezi Beach, Dar es Salaam, Mwakyembe alisema ana matumaini makubwa ya Kilimanjaro Stars kurejea na ubingwa kutokana na ubora wa wachezaji wanaounda kikosi hicho.
Mwakyembe alisema anafahamu kati ya timu zinazoshiriki michuano hiyo, inayozungumzwa zaidi ni Tanzania, hivyo ni jukumu la wachezaji kujituma na kuibuka na ushindi kila mechi watakayocheza.
“Nina matumaini makubwa na kikosi hiki, nimeangalia idara zote zimekamilika hasa safu ya ushambuliaji nimemwona Kichuya hapa na Ajib, naamini hamtawaangusha Watanzania, pigeni kila mtakayekutana naye,” alisema Mwakyembe.
Alisisitiza kuwa jambo la msingi ni kuzingatia nidhamu na kutodharau timu yoyote, kwani kila mechi ichukuliwe kama fainali au wanacheza na Brazil.
Katika hatua nyingine, Mwakyembe alitoa ahadi ya kwenda Kenya kuishangilia timu hiyo, endapo itafanikiwa kushinda mechi mbili mfululizo wakianzia na Libya.
Kwa upande wake Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia, ameahidi kutoa ‘bonasi’ kwa kila hatua timu hiyo itakayotinga, lengo ni kuhamasisha wachezaji waweze kuwafurahisha Watanzania.
Kocha mkuu wa timu hiyo, Ammy Conrad ‘Ninje’, alisema maandalizi yamekamilika, atakapofika watafanya mazoezi ya mwisho kwa siku mbili kabla ya kuwavaa Libya.
“Tupo tayari kwa michuano, tumejipanga kupambana kila mechi kwani hilo linawezekana kwa sababu tunachotaka ni kuchukua ubingwa wa michuano hiyo,” alisema Ninje.
Alisema amebadilisha mfumo wa uchezaji na anatumia ‘Diamond System’ yaani 4:4:2 huku akibadilisha kulingana na aina ya mchezo.
Tanzania imepangwa Kundi A pamoja na Libya, Rwanda, Zanzibar na wenyeji Kenya.
Tupe Maoni Yako