Saturday, December 9, 2017

Mawingu Tz

Soma anachojivunia kocha Kilimanjaro licha ya kuboronga

PAMOJA na matokeo mabaya ya kufungwa mchezo wa pili mfululizo baada ya kutoka sare na Libya, kocha wa timu ya taifa ya Tanzania bara ‘Kilimanjaro Stars’ Ammy Ninje amesema anafurahishwa na kiwango cha wachezaji wake.
Akizungumza mara baada ya mchezo wa leo ambao wamefungwa mabao 2-1 na timu ya taifa ya Rwanda ‘Amavubi’, Ammy amesisitiza kwamba anachojivunia katika michuano hiyo licha ya kufanya vibaya ni kiwango bora cha wachezaji wake.
“Vijana wamecheza vizuri sana, nimeridhishwa na kiwango walichoonyesha, najivunia vijana wangu,” alisema Ammy.
Mfungaji wa bao pekee la Kilimanjaro Stars, Danny Lyanga akipiga mbele ya mchezaji wa Rwanda
Magoli ya Rwanda katika mchezo huo yamefungwa na Innocent Nshuti dakika 17 na Abbedy Biramahire dakika 65 huku lile la kufutia machozi la Kilimanjaro likifungwa na Danny Lyanga dakika ya 29.
Kauli hiyo la Ammy inaweza kuwashangaza wengi kwani Kilimanjaro wamebakiza mechi moja tu dhidi ya Kenya, mchezo ambao bado hauwezi kutoa matumaini makubwa kwani hata wakishinda watafikisha pointi nne sawa na Rwanda iliyomaliza michezo yake minne na endapo Kenya watashinda leo dhidi ya Zanzibar basi Stars watakuwa wameaga rasmi.
Zanzibar wanaongoza kundi hilo baada ya kufikisha pointi sita, wenyeji Kenya wakiwa wa pili kwa pointi nne sawa na Rwanda, Libya ina pointi tatu na Kilimanjaro ikiburuza mkia ikiwa na pointi moja

Tupe Maoni Yako