Friday, December 1, 2017

Mawingu Tz

Mzamiru Yassin Awalegezea Yanga, Simba Wanuna

HII kwa Simba haijakaa vizuri, ni ngumu kumeza. Mzamiru Yassin amethibitisha kwamba kama Yanga wakimwekea mezani Sh70 milioni, anasaini kwao bila wasiwasi.
Lakini pamoja na fungu hilo, Wana Jangwani watalazimika kumwongezea gari ndogo ya kishua pamoja na kumpangishia nyumba.

Kwa mujibu wa nyota huyo dau hilo ndilo linaloweza kumfanya amwage wino kwa klabu za hapa ndani, huku akisema nje ya nchi dili lake likitiki makubaliano yatakuwa mengine.
Habari kutoka kwa mtu wa karibu wa mchezaji huyo, zinadai kwamba ameshafanya mazungumzo na Yanga na Azam ambao walimwibukia geto kwake mitaa ya Magomeni, Dar es Salaam.
Lakini habari hizo ambazo Mzamiru anazikanusha zinasema kwamba hakuzungumza nao kwa kirefu, kwa kuwa kuna ishu ya nje ya nchi anaisikilizia, huku kukiwa na habari kwamba hayuko vizuri na watu wa Simba kwani alichukia walivyozuia dili lake la Oman wakitaka fungu kubwa.Klabu ya Al Rustaq ya Oman ndiyo imeelezwa kufanya mazungumzo na Simba, lakini yakaishia juu kwa juu kwa viongozi, ingawa Mzamiru alishtukia.

“Bado nina mkataba wa miezi sita na Simba, ila ukimalizika tu klabu inayohitaji huduma yangu, iwe na Milioni 70, ininunulie gari pamoja na kunipangia nyumba ya kuishi, kuhusu mshahara ni makubaliano ya siri baina yangu na wahusika,” alisema mchezaji huyo.
“Hata klabu yangu ya Simba ikiwa na dau hilo nitakuwa tayari kuitumikia, kwani soka kwangu ni kazi ambayo nimeichagua kwa ajili ya kuendesha maisha yangu,” alisema.
Mzamiru alisema licha ya kubakiza miezi sita Simba, ataendelea kujituma kwa bidii na kuongeza ushindani katika namba yake na hamu yake kubwa ni kuona klabu hiyo inatwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu.

“Natamani kuwa mmoja wa wale ambao watachukua ubingwa wa ligi ndani ya kikosi cha Simba, msimu uliopita tulichukua Kombe la FA na hivyo tumeanza kazi ya kurejesha vikombe klabuni kwetu,” alisema Mzamiru aliyeibukia kuwa kipenzi cha mashabiki.
Katika fainali ya FA Simba iliibuka kidedea kwa kuifunga Mbao FC mabao 2-1.

Tupe Maoni Yako