KIUNGO wa Singida United ya Singida, Mudathir Yahaya amechaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa Novemba wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu wa 2017/2018.
Mudathir ameshinda tuzo hiyo baada ya kuwazidi wenzake wawili, beki Asante Kwasi wa Lipuli ya Iringa na mshambuliaji Danny Usengimana wa Singida United pia, alioingia nao fainali ya kuwania nafasi hiyo.
Katika uchambuzi uliofanywa Dar es Salaam wiki hii kwenye kikao cha Kamati ya Tuzo za VPL zinazotolewa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kutokana na mapendekezo kutoka kwa makocha waliopo viwanja mbalimbali ambavyo ligi hiyo inachezwa msimu huu.
Mchezaji huyo alitoa mchango mkubwa kwa Singida United mwezi huo ikipata pointi saba katika michezo mitatu iliyocheza na kupanda katika msimamo wa ligi kutoka nafasi ya sita iliyokuwepo mwezi Oktoba hadi ya nne.
Singida United ilitoka 0-0 na Yanga, iliifunga Mbeya City mabao 2-1 na pia iliifunga Lipuli bao 1-0, ambapo Mudathir anayecheza nafasi ya kiungo alicheza dakika zote 270 sawa na michezo mitatu na hakuwa na kadi yoyote.
Alitajwa mchezaji bora wa mchezo wa Singida United na Yanga uliofanyika Uwanja wa Namfua, Singida, alicheza kwa kiwango cha juu wakati Singida United ilipochuana na Lipuli, pia alisaidia kutengeneza nafasi ambazo zilitumiwa vyema na wenzake katika kupata ushindi dhidi ya Mbeya City, huku yeye akihusika kwa kwa kiasi kikubwa kupambania ushindi huo.
Mafanikio yake kwa mwezi huo yalisaidia kumrudisha katika kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ na kile cha Zanzibar ‘Zanzibar Heroes’, ambacho kinashiriki michuano ya Chalenji inayoendelea nchini Kenya.
Kampuni ya Vodacom, ambao ndiyo wadhamini wa ligi hiyo ina utaratibu wa kuwazadiwa wachezaji bora wa kila mwezi, huku pia mwisho wa msimu kukiwa na tuzo mbalimbali zinazohusu ligi hiyo, ambapo msimu wa mwaka 2016/2017 kulikuwa tuzo 16 zilitolewa kwa washindi wa kada mbalimbali.
Mudathir atazawadiwa Sh milioni moja kutoka Vodacom pamoja na kisimbusi (decoder) cha Azam kwa kuibuka Mchezaji Bora wa mwezi.
Tupe Maoni Yako