Wednesday, December 20, 2017

Mawingu Tz

Mavugo Karudi Aisee, Simba Yafunguka

Mshambuliaji, Laudit Mavugo yuko njiani kurejea nchini huku akisisitiza anarudi kujua hatma yake na Simba ingawa uongozi wa klabu hiyo umesisitiza haujamuacha.
Akizungumza na kutoka jijini Nairobi, mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Burundi, alisema anarejea Dar es Salaam kujua hatma yake.
Awali, kulikuwa na tetesi za mchezaji huyo aliyeng'ara kwenye Ligi Kuu ya Burundi kabla ya kutua Simba kwamba anapelekwa kwa mkopo Oman, lakini mwenyewe amesisitiza endapo ataondoka Simba anataka kucheza soka Kenya.
"Sina taarifa za kupelekwa Oman, nimemaliza mashindano ya Chalenji niko njiani kurudi Dar es Salaam ili kujua hatma yangu na Simba, lakini narudia tena napenda kucheza Ligi ya Kenya na nimeanza mazungumzo na timu ya Gor Mahia na AFC Leopards.
Mazungumzo yakienda vizuri nitajiunga na mojawapo ya timu hizo, naamini Ligi ya Kenya itanifungulia njia ya kufika mbali zaidi kisoka," alisema Mavugo aliyetua Simba kwa mbwembwe.
Kocha wa Gor Mahia, Dylan Kerr ameonyesha nia ya kumjumuisha kwenye kikosi chake Mrundi huyo ingawa Simba nayo inasisitiza haijamuacha mchezaji huyo ambaye hakuwa na msimu mzuri tangu ajiunge na klabu hiyo kutoka Vital'O ya Burundi.
Hata hivyo, kwenye usajili wa dirisha dogo Simba imewaongeza katika kikosi Dayo Antonio wa Ferroviario na Mghana Asante Kwasi, hivyo kufikisha idadi ya wachezaji saba ingawa usajili wa Kwasi bado una utata kufuatia Lipuli kudai ni mchezaji wao na itamuwekea pingamizi TFF.
Kaimu Rais wa Simba, Salim Abdallah 'Try Again' alisema usajili wa Kwasi haujakamilika na mazungumzo yanaendelea huku akifafanua klabu hiyo pia haijamuacha Mavugo.
"Hatujasema tumemuacha Mavugo, bado ni mchezaji wetu na ataendelea kuwepo kwenye kikosi chetu, mashabiki wetu wawe na subira siku si nyingi tutatoa ripoti rasmi ya usajili, lakini Mavugo bado tuko naye," alisema bosi huyo wa Simba.
Ingawa hatma ya Mavugo kubaki Simba kama uongozi unavyosisitiza itategemea na maelewano ya Simba na Lipuli kuhusu usajili wa Kwasi ambaye kama atafanikiwa kujiunga na mabingwa hao wa Kombe la FA basi atafikisha idadi ya wachezaji saba wa kigeni na Mavugo hatakuwa na nafasi zaidi ya kuondoka Simba.

Tupe Maoni Yako