Thursday, December 28, 2017

Mawingu Tz

Umesikia Alichokisema Kwasi? Atoa Kali Ya Funga Mwaka Simba


BEKI Mghana, Asante Kwasi, amewaambia mashabiki wa Simba kwamba hakwenda katika kikosi chao kuuza sura, bali ni kuwafanyia kazi ambayo itawafanya wasijute kumsajili.
Kwasi ametua Simba katika kipindi hiki cha usajili wa dirisha dogo akitokea Lipuli ya Iringa, japo uhamisho wake ulikumbwa na bonge la zengwe.
Baada ya tetesi za Simba kumsajili Kwasi kuzagaa nchini, Lipuli walikuja juu wakisisitiza mchezaji huyo kuwa mali yao, akiwa bado hajafikisha muda wa kufanya mazungumzo na klabu yoyote ile bila kuwasiliana nao kama walivyofanya Wekundu wa Msimbazi hao.
Kwa mujibu wa kanuni za usajili, mchezaji yeyote anaweza kufanya mazungunzo na klabu nyingine inayomtaka iwapo tu atakuwa amebakiza si zaidi ya miezi sita katika mkataba na klabu yake.
Baada ya kubaini ‘walibugi’, Simba walikubali yaishe kwa kukutana na uongozi wa Lipuli na mwisho wa siku, kukubaliana na kumtwaa kwa dau la Sh milioni 25.
Akizungumza na BINGWA jana, Kwasi alisema amefurahi mno kutua Simba, kwani ni klabu aliyokuwa amepania mno kuitumikia hapa nchini.
Aliwataka mashabiki wa timu hiyo kumpa sapoti ya kila aina ili aweze kutimiza majukumu yake kadiri ya uwezo wake, akiamini ana uwezo wa kuongeza kitu ndani ya kikosi hicho.
“Nawaomba mashabiki wa Simba, wanisapoti na kuniamini, naahidi kutimiza majukumu yangu ambayo yamenipeleka hapo, nitatumia uwezo na juhudi zangu zote, kikubwa ni ushirikiano wao na kwa uwezo wa Mungu, kila kitu kitafanikiwa,” alisema Kwasi.
Akiizungumzia safu ya ulinzi katika kikosi chake hicho kipya, alisema anatambua anakwenda kukutana na wachezaji wazuri lakini atapambana kuhakikisha anapata nafasi kwenye kikosi cha kwanza.
Katika safu hiyo ya ulinzi, Kwasi anakwenda kukutana na akina Salim Mbonde, Jjuuko Murushid, Yusuph Mlipili na Paul Bukaba, ambapo atatakiwa kukaza buti ili kumshawishi kocha amuamini na kumpanga kikosi cha kwanza.

Tupe Maoni Yako