Pamoja na Simba, Yanga na Azam kusheheni mastaa katika vikosi vyao kila idara bado kuna wachezaji wakibanwa tu timu hizo hazipatia matokeo.
Simba inaongoza Ligi Kuu Tanzania Bara kwa pointi zao 23 sawa na Azam iliyopo nafasi ya pili wakitofautiani mabao ya kushinda, Yanga ipo nafasi ya tatu na pointi 22.
Si Simba,Yanga wala Azam aliyeonja radha ya kufungwa katika michezo 11 ya mwanzo wa Ligi Kuu zaidi ya kupata sare tu.
Inawezekana Azam, Yanga na Simba kupoteza michezo yao ya ligi kama zitabanwa kwenye maeneo yake hatari ambayo yamekuwa yakitumika kujipatia matokeo.
Mtandao huu umeangalia maeneo ambayo wakibandwa basi ni rahisi kupata matokeo.
Simba (Kichuya na Nyoni)
Ubora wa Simba umechangiwa mno na uwepo wa Shiza Kichuya na Erasto Nyoni upande wa beki ya kulia.
Licha ya Simba kuwa na Emmanuel Okwi anayeongoza kwa ufungaji hawezi kuithiri timu hiyo kupata matokeo hata kama asipokuwepo au akidhibitiwa, mabao mengi ya Okwi ameyafunga kwenye mechi chache hasa za mkoani hapa.
Kichuya ameipa Simba pointi 7 kati ya 23 walizonazo, ukiondoa mabao ambayo amefunga Okwi katika michezo ambayo amecheza bado Simba ilikuwa kwenye mazingira ya kupata ushindi, Kichuya mwenye mabao 5, ameifungia timu hiyo mabao muhimu zaidi.
Oktoba mosi, Kichuya alifunga bao la kwanza kwenye ushindi ambao Simba iliupata wa mabao 2-1 dhidi ya Stand United, pia aliibeba timu yake katika mchezo dhidi ya Yanga, ambao ulimalizika kwa sare ya bao 1-1, kisha akaja kuipa pointi tatu katika ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mbeya City, ugenini.
Simba inanguvu kubwa upande wa kulia ambao amekuwa akicheza Nyoni, beki huyo wa kulia amekuwa akifanya vizuri majukumu yake kwenye kuzuia pamoja na kushambulia, mabao mengi ya Simba yamechangiwa na Nyoni upande wake wa kulia.
Kama Kichuya na Nyoni watabanwa kwa kutopewa nafasi ya kucheza basi sio ajabu kuona Simba ikipoteza au hata ikisota kupata matokeo ya ushindi kutokana na umuhimu wa wachezaji hao ambao wamechangia zaidi ya asilimia 60 kwenye upatikanaji wa matokeo ya Simba.
Yanga (Ajib na Chirwa)
Wakati Yanga ikisumbuliwa na majeraha ya washambuliaji wake Donald Ngoma na Amis Tambwe, ni Ibrahim Ajib na Obrey Chirwa ambao wanaonekana kuwa tegemeo kwenye kikosi hicho kuanzia kwenye utengenezaji nafasi ya mabao hadi kwenye ufungaji.
Ajib aliyesajiliwa na Yanga akitokea Simba mwanzoni mwa msimu huu wa 2017/2018 ameingia moja kwa moja kwenye mfumo wa kocha mkuu wa timu hiyo,George Lwandamina yote hiyo ni kutokana na uwezo wake wa kutengeneza mabao na kufunga.
Ufundi wa Ajib umeinufaisha Yanga kupata pointi 12 kati ya 21, kama sio Ajib ni wazi Yanga ingekuwa kwenye hali mbaya kutokana na mabao yake muhimu ambayo alianza kuyafunga kwenye mchezo dhidi ya Njombe Mji ambapo Yanga ilishinda kwa bao 1-0.
Pia akaja akafunga tena bao moja kwenye mchezo dhidi ya Ndanda ambao nao Yanga ilishinda kwa bao 1-0,Ajib aliendelea kuibeba tena Yanga kwenye ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Kagera Sugar ambapo alifunga bao la ushindi na la pili kwa mabingwa hao watetezi.
Ajib alichangia tena ushindi ambao Yanga iliupata wa mabao 4-0 dhidi ya Stand United kwa kufunga mara mbili,ukiona Ajib hajafunga basi huenda akawa ametengeneza nafasi ya bao.
Mshambuliaji pekee ambaye anaongoza kwa kufunga mabao mengi kwa Yanga ni Chirwa ambaye ameifungia timu hiyo mabao 6, kama Chirwa na Ajib wanadhibitiwa kwa kunyimwa nafasi ya kufanya watakacho na mpira basi Yanga itaanza kumtafuta mchawi kwenye kikosi chao.
Azam (Mbaraka)
Ni kwa muda mrefu Azam imekuwa na tatizo kwenye eneo lake la mwisho la ushambuliaji kwa kushindwa kupata ushindi mnono kwenye michezo yake hata hivyo katika mazingira hayo ni Mbaraka Yusuph ambaye amekuwa akiibeba timu hiyo walau kupata matokeo ya ushindi mwembamba.
Mbaraka amechangia upatikanaji wa pointi 9 kwenye kikosi cha Azam kwa mabao yake matatu ambayo ameyafunga kwenye michezo dhidi ya Kagera Sugar, Lipuli na Mbeya City ambapo timu yake imeshinda michezo yote hiyo kwa bao 1-0.
Labla ujio wa mshambuliaji, Bernard Arthur aliyesajiliwa akitokea Liberty Professionals Accra ya Ghana huenda ukaongeza upana wa makali katika eneo la ushambuliaji la timu hiyo.
Lakini mpaka sasa mchezaji muhimu zaidi kwenye kikosi cha Azam ni Mbaraka ambaye kama atanyimwa nafasi ya kufunga basi huenda sare kwa Azam zikaendelea kutawala.
-Mwanaspoti
Tupe Maoni Yako