HATIMA ya mshambuliaji wa PSG, Neymar, imekuwa ikitamba kwenye vichwa vingi vya habari kwa muda wa siku kadhaa sasa ambapo linalozungumziwa sana ni Mbrazili huyo kwenda Real Madrid.
Yaani kuhamia kwa mahasimu hao wakubwa wa klabu ya Barcelona, timu ya zamani ya Neymar kabla hajaenda PSG.
Hata hivyo, nyota huyo aliyetua Paris kwa dau lililoshtua wengi, bado anaendelea kusisitiza kwamba ataendelea kuitumikia timu yake ya sasa ya PSG hadi majira ya kiangazi ya mwaka 2019.
Vyombo vingi vya habari kwa sasa vinamfuatilia sana Neymar na kumpiga maswali juu ya tetesi zinazoendelea kuzagaa kuwa atasaini mkataba wa kuichezea Madrid, lakini mshambuliaji huyo ameendelea kukomaa na msimamo wake kwamba hakitatokea kitu kama hicho.
Msimamo wa Neymar hadi leo ni kubaki Paris kwa angalau miaka miwili na haoneshi dalili yoyote ya kwenda tofauti na alichodhamiria.
Aidha, vigogo wa Madrid nao wameamua kuishi kwenye maneno ya Neymar, ila bado hawajapotezea dili la kumchukua nyota huyo.
Lakini kwa sasa, mabingwa hao mara 12 wa Ulaya wameamua kusubiri hadi majira ya kiangazi kama alivyosema Neymar, 2019!
Hizi nazo ni sababu nyingine zinazowapa Madrid nguvu ya kumsubiria Neymar.
Mosi, watakuwa na uwezo wa kumsajili Neymar bila kuvunja mkataba wake kwa gharama kubwa (clause).
Kwa namna yoyote ile, wafanikiwe au wafeli kumsajili Neymar, Real Madrid wanaamini kuwa hadi 2019 dili hilo litafanikiwa tu kwa kuwa tayari ameshaamua kubaki Paris na Cristiano Ronaldo ndiye supastaa wa klabu na asiyetaka kusikia mshambuliaji mwingine akisajiliwa hivi karibuni.
Pili, na mwisho, Bale anarudi kuja kuchukua nafasi yake.
Tayari ameshapona na ana hamu kweli ya kuisaidia timu, lakini bado hamu hiyo haitawahadaa Madrid katika mpango wao wa kumsajili Neymar, sababu kuu ni majeraha yake ya mara kwa mara.
Hata hivyo, kuna taarifa nyingine inayosema kuwa Madrid wanajipanga kusaka daktari atakayeweza kugundua nini hasa kinachopelekea mkali huyo aumie kila mara na kulimaliza kabisa kama ikiwezekana.
Tupe Maoni Yako