Saturday, December 9, 2017

Mawingu Tz

Kocha Omog Ampa Kazi Nzito Hanspoppe..Ni Kuhusu Usajili Wa Wachezaji

UKISIKIA mtego basi ndio huu. Kocha Mkuu wa Simba, Mcameroon Joseph Omog, ameipa muda wa siku tano Kamati ya Usajili ya klabu hiyo chini ya Mwenyekiti wake, Zacharia Hanspoppe, kuisuka upya timu hiyo kwa kuzingatia mapendekezo yake.
Omog anayeifundisha Simba kwa mwaka wa pili sasa, yupo kwao kwa mapumziko, lakini ameisisitiza kamati hiyo isajili nyota wapya aliowapendekeza ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kuwania taji la Ligi Kuu Bara na mechi za Kombe la Shirikisho barani Afrika.
Kocha huyo aliyewahi kutwaa Kombe la Shirikisho akiwa na AC Leopard ya Congo, ameitaka kamati hiyo kufanya kazi kwa haraka ili atakaporejea Alhamisi ijayo aanze kazi moja kwa moja.
Katika ripoti yake, Omog alitaka asajiliwe kipa, beki wa kati anayeweza pia kucheza pembeni, winga na straika mmoja mwenye uwezo mkubwa wa kufumania nyavu kuliko John Bocco na Laudit Mavugo waliopo kikosini humo kwa sasa.
Mabosi wa Simba tayari wamemleta nchini straika Mzambia, Jonas Sakuhawa ambaye anafanya majaribio huku wakiwa kwenye mazungumzo na winga wa Mwadui, Hassan Kabunda lakini Omog amesisitiza mambo yakamilike haraka.
“Nawafahamu wachezaji wote wa ndani ndiyo maana nimeomba kamati ikamilishe usajili mapema,” alisema Omog ambaye msimu uliopita aliisaidia Simba kushinda taji la FA.
Meneja wa Wana Msimbazi hao, Robert Richard, alisema kamati ya usajili inaendelea na vikao vya mara kwa mara huku wakiwa wapo katika mazungumzo ya karibu na wachezaji wote waliopendekezwa na kocha.
“Nawasiliana na kocha Omog mara kwa mara na kumueleza asiwe na wasiwasi, kamati ya usajili inafanya kazi yake kwa kasi sana na atakaporudi nchini atakuta mambo yapo safi,” alisema Richard.

WANNE WAZUIWA
Wakati huo huo, mabosi wa Simba wamewatuliza nyota wanne waliotaka kutimka klabuni hapo kwa maelezo kwamba bilionea Mohammed Dewji ‘MO’ aliyeshinda zabuni ya kuwa mwekezaji mkubwa klabuni hapo, ametaka nyota muhimu yeyote asiachwe.
Mastaa wanne wa Simba ambao ni Jamal Mwambeleko, Juma Liuzio, Jamali Mnyate na Laudit Mavugo wameomba kuvunjiwa mikataba yao kwa makubaliano maalumu, lakini mabosi hao wa Simba wamewatolea nje katika jambo hilo.
“Nimewafuata viongozi kuomba waniache nikaanze maisha mapya Singida United, lakini wamenikatalia na kuniambia nisahau hilo,” alisema Liuzio.
“Niliwasiliana na viongozi wakasema ndio kwanza nina nusu msimu katika mkataba wangu kwahiyo kuhusu kuondoka hapa Simba nisifikirie hata kidogo,” alisema Mwambeleko.
-Mwanaspoti

Tupe Maoni Yako