Saturday, December 9, 2017

Mawingu Tz

Yanga Ikiwapata Mastaraika Hawa....Hata Aje Mwarabu Hatoki

GEORGE Lwandamina amezichungulia timu atakazoenda kuvaana nazo Ligi ya Mabingwa Afrika mwakani na kugundua hakuna namna zaidi ya kuifanya Yanga iwe ya kibabe.
Kwanza amewaambia mabosi wake wasajili vichwa vya maana, kisha akawataka waandae mkwanja wa nguvu kuweza kuhimili mikikimikiki ya vigogo hao watakaokabiliana nao.
Baadhi ya vigogo wanaoweza kukutana na Yanga ni Al Ahly au Misr Lel Makkasa za Misri, Esperence au Etoile du Sahel za Tunisia, TP Mazembe, AS Vita (DR Congo) na ES Setif na MC Alger (Algeria).
Pia kuna Bidvest Wits, Mamelodi Sundowns (Afrika Kusini), watetezi Waydad Casabalanca au Difaa El Jadidi (Morocco), Al Hilal, Al Merreikh (Sudan), Zesco United au Zanaco (Zambia), Stade Malien au AS Real Bamako (Mali)
Timu nyingine ni Asec Memosas ya Ivory Coast ambayo ni moja ya klabu 10 zilizobeba taji hilo la Afrika.
Kwa vigogo hao, kocha huyo anaamini wakijiandaa kizembe itakula kwao, ndio maana fasta wakasajiliwa Fiston Kayembe kutoka DR Congo na Yohana Mkomola na kuwazuia nyota wake wote wasiondoke kikosini.
Lakini kama haitoshi, akasisitiza aletewe mastraika wengine wawili wa kigeni ambao wapo njiani kutua nchini ili kuliwahi dirisha dogo la usajili litakalofungwa Ijumaa ijayo.
Mzambia huyo amesema kilichobaki kwa sasa kwa mabosi wake ni kuhakikisha wanatekeleza kile alichowafahamisha mapema na hata wakiletewa Mwarabu naamini watampiga tu kwa mziki alionao kwa sasa..

FUNGU MAALUMu
Akizungumza na Mwanaspoti, Lwandamina alisema kuwa hatua ya kwanza amegundua timu nyingi zilizofuzu zina nguvu kubwa ya fedha, hivyo mabosi wake kabla ya kufanya lolote wanatakiwa kuangalia uwezo wa mfuko wao.
Lwandamina alisema kutokana na nguvu zao za fedha, klabu hizo zinaweza kusajili wachezaji wanaohitajika katika mashindano hayo ambapo kwake ndio maana bado anataka kuona baadhi ya nyota wanapatikana katika kikosi chake.
Mzambia huyo alisema hana wasiwasi katika ubora wa kikosi chake katika mashindano ya ndani, lakini kama mipango ya kifedha haitakaa sawa inaweza kumpa wakati mgumu mbali na mipango yake ya kuona upana wa kikosi chake.
“Nimeziona hizo timu nazijua si kwa kubahatisha ni timu ngumu, lakini ubora wao zaidi unatokana na nguvu ya fedha wanajua kutumia fedha kufanya maandalizi yaliyobora kabla ya mashindano,” alisema Lwandamina.
“Najua tutashindana nao, japo sijajua tutakutana na timu zipi ila katika maandalizi ni bora tukaangalia kwa ujumla washindani wetu, tunahitaji kuangalia upana na ubora wa kikosi chetu nafikiri hapa ndiyo kwenye kazi.

JEURI IPO HAPA
Ukiondoa nyota wapya wanaoingia, Lwandamina anajivunia kuwa na wakali kama Mkameruni Youthe Rostand, mabeki Kelvin Yondani, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Juma Abdul, Andrew Vincent ‘Dante’’, viungo Thabani Kamusoko, Kabamba Tshishimbi, Rafael Daud, Pius Buswita na mastraika Ibrahim Ajib, Obrey Chirwa, Emmanuel Martins pamoja na Geofrey Mwashiuya.

TSHISHIMBI KARUDI
Kati ya mambo yaliyomfurahisha Lwandamina ni kurejea kikosini kwa kiungo wake, Kabamba Tshishimbi ambaye jana Ijumaa aliripoti mazoezini ikielezwa amepona maumivu yake.
Katika mazoezi hayo, kiungo huyo alikimbia peke yake nje ya uwanja ikiwa ni kutekeleza programu wanayopewa wachezaji wanaoanza mazoezi kikosini humo wakitokea benchi la majeruhi.
-Mwanaspot

Tupe Maoni Yako