HUKU mashabiki wa soka, hasa wa Liverpool wakijiuliza ni mchezaji gani hatari zaidi kati ya Luis Suarez aliyeondoka na Mohamed Salah, kocha Jurgen Klopp amesema asihusishwe katika mjadala huo.
Klopp amesema havutiwi na namna wachezaji hao wanavyofananishwa, akisema hiyo ni kazi ya magazeti na mitandao ya kijamii, hivyo haimhusu.
Salah, raia wa Misri, amekuwa moto wa kuotea mbali tangu alipojiunga na Liver, kwani ameshaipachikia mabao 17 tangu kuanza kwa msimu huu, yakiwamo mawili aliyotupia Jumatano ya wiki hii katika ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Stoke City.
Makali hayo yamewafanya mashabiki kuanza kumfananisha na Suarez, ambaye kwa misimu mitatu na nusu aliyokaa Anfield kabla ya kwenda Barcelona mwaka 2014 alikuwa amecheka na nyavu mara 82.
Kwa upande wake, Klopp alisema anavutiwa na kiwango cha sasa cha Salah, lakini asingependa kumfananisha na Suarez, kwani ni mchezaji anayemheshimu pia.
“Sivutiwi (kuwafananisha). Namheshimu sana Suarez, ni lejendari wa Liverpool,” alisema Klopp, kuwaambia waandishi wa habari kuelekea mchezo wake wa jana dhidi ya Brighton.
“Ni bonge la mchezaji, napenda aina yake ya uchezaji, lakini kwa sasa si mchezaji wa Liverpool.
“Kazi yangu si kulinganisha wachezaji au mchango wao kikosini. Hiyo ni kazi ya magazeti au mitandao ya kijamii. Huwa sivutiwi na mjadala huo.”
Salah alisajiliwa na Liver kwa Pauni milioni 39 baada ya kung’ara Serie A, ambako alipachika mabao 29 katika mechi 65 alizokuwa na ‘uzi’ wa Roma,
Suarez naye amekuwa kwenye kiwango cha juu tangu alipotua Barca, akiwa ameshaifungia timu hiyo ya Catalunya jumla ya mabao 90, huku akiwa ameingia uwanjani zaidi ya mara 100
Tupe Maoni Yako