Friday, December 8, 2017

Mawingu Tz

Njombe Mji Yasajili Wawili Wa Mtibwa Sugar, Yataka Wengine Wawili Kwa Kutoka Yanga


TIMU ya Njombe Mji FC imeimarisha kikosi chake kwa ajili ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kwa kusajili wachezaji wawili chipukizi kwa mkopo, beki Nickson Kibabage na kiungo Muhsin Malima kutoka Mtibwa Sugar ya Morogoro. 

Kocha wa Njombe Mji FC, Mlage Kabange amesema  kwamba wamekwishamalizana na Mtibwa Sugar kuhusu wachezaji hao na tayari wameanza safari kuelekea Njombe.
“Wako njiani wanakuja (Kibabage na Malima) baada ya sisi kumalizana na klabu yao (Mtibwa Sugar). Ni vijana wadogo ambao tunatarajia wataisaidia sana timu katika mechi zijazo za Ligi Kuu,”amesema Kabange winga wa zamani wa Simba SC ya Dar es Salaam.


Wote, Kibabage na Malima walikuwemo kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys kilichoshiriki Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON U-17) Mei mwaka huu nchini Gabon.
Pamoja na wawili hao wa kutoka Mtibwa Sugar, Kabange pia amesema bado wanasubiri majibu kutoka klabu ya Yanga juu ya maombi ya kuwachukua kwa mkopo pia, kiungo Yussuf Mhilu na mshambuliaji Matheo Anthiny Simon.
“Tumewaandikia barua Yanga kuwaomba watupe wachezaji wawili kwa mkopo, Yussuf Mhilu na Matheo, lakini bado hawajatujibu, hivyo bado tunasubiria majibu yao,”amesema. 


Tupe Maoni Yako