BEKI wa timu ya Kagera Sugar, Mohammed Fakhi, amesema kama kocha wao, Mecky Mexime, ataboresha eneo la kiungo na safu ya mshambuliaji, kikosi hicho kitafanya vizuri katika mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara na kutengeneza nafasi nyingi za kufunga.
Akizungumza na BINGWA, Fakhi alisema kikosi kilichopo ni kizuri hasa kutokana na uwepo wa wachezaji wengi wenye uzoefu, lakini wakisajili kiungo na mshambuliaji wa kusaidiana na wengine timu itafanya vizuri katika mechi zilizobaki.
“Tulianza vibaya Ligi Kuu lakini tunamshukuru Mungu tumepata matokeo ambayo yametupa matumaini, kilichobaki kwa sasa ni kupambana kuongeza kasi ya mabao,” alisema.
Fakhi hajacheza mechi yoyote msimu huu kutokana na kusumbuliwa na majeraha ya mkono, ambapo akizungumzia afya yake alisema anaendelea vizuri na tayari ameanza mazoezi na anatarajia kujiunga na wenzake.
“Ligi ilivyoanza nilienda kambini lakini sikuwa fiti kwa mazoezi magumu kutokana na maumivu ya mkono, sasa hivi nafanya mazoezi ya aina zote ndio maana nataka kurudi kuisaidia timu yangu,” alisema.
Wakati huo huo, mshambualiaji Atupele Green, amerejea kuichezea timu hiyo na kusaini mkataba wa miezi sita baada ya kuachana na Singida United.
Akizungumza na BINGWA, Atupele alisema anajisikia furaha kurudi kuitumikia Kagera kwa sababu ni kama anarejea nyumbani, hivyo anaamini wachezaji wenzake watampokea vizuri.
“Lazima ujisie vizuri unaporejea nyumbani au sehemu uliyozoeleka, wakati nacheza Kagera nilifanya vizuri lakini pia naamini nikirudi nitafanya hivyo kwa kushirikiana na wenzangu,” alisema.
Tupe Maoni Yako