SIMBA SC itafungua dimba na URA ya Uganda katika michuano maarufu ya Kombe la Mapinduzi, Januari 2, mwaka 2018 Uwanja wa Amaan, Zanzibar mchezo ambao utaanza Saa 2:15 usiku.
Mahasimu wao, Yanga wataanza na JKU ya Zanzibar Desemba 1, Uwanja wa Amaan pia, mchezo ambao nao utaanza Saa 2:15 usiku.
Mabingwa watetezi, Azam FC wataanza na Jamhuri katika mchezo utakaofanyika Uwanja wa Amaan pia Desemba 2, lakini kuanzia Saa 10:15 jioni. Ufunguzi rasmi wa Kombe la Mapinduzi 2018 utafanyika Desemba 30, mwaka huu kwa mechi mbili kuchezwa Uwanja wa Amaan, kwanza Zimamoto na Mlandege Saa 10:17 jioni na baadaye JKU na Shaba Saa 2:15 usiku.
Simba imepangwa Kundi A pamoja na Azam FC, Jamhuri, Taifa ya Jang’ombe na URA ya Uganda, wakati Yanga imetupwa Kundi B pamoja na JKU, Mlandege, Zimamoto na Shaba.
Simba itamenyana na Azam FC Januari 6, ikitoka kukipiga na Taifa ya Jang’ombe Januari 4, kabla ya kumalizia mechi zake za Kundi A Januari 8 na Jamhuri.
Azam FC itacheza na Taifa ya Jang’ombe Januari 4 kuanzia Saa 10:15, kabla ya kumenyana na Simba na itahitimisha mechi zake za Kundi A kwa kuumana na URA Januari 8 Saa 10;15 pia jioni Uwanja wa Amaan.
Baada ya mechi na JKU, Yanga watarudi tena uwanjani Januari 3 kwa mchezo na Shaba, Januari 5 na Zimamoto kabla ya kukamilisha mechi zake za Kundi B kwa kumenyana na Mlandege Janauri 7 Uwanja wa Amaan.
Nusu Fainali zinatarajiwa kuchezwa Januari 10 na Fainali itakuwa Januari 13, mwaka 2018 Uwanja wa Amaan kuanzia Saa 2:15 usiku.
Tupe Maoni Yako