KOCHA Mkuu wa Yanga, Mzambia, George Lwandamina, juzi Jumatatu aliondoka kwenda kwao Zambia kwa ajili ya mapumziko baada ya Ligi kuu Bara kusimama kwa muda kupisha michuano ya Kombe la Chalenji itakayoanza Jumapili hii nchini Kenya.
Lwandamina ameondoka Yanga ikiwa ni baada ya kuwapa mapumziko ya siku kumi wachezaji wa kikosi hicho ambao nao bila ya kuchelewa, wametimka kwenda kuona familia zao.
Akizungumza na Chandimu , Lwandamina alisema baada ya mapumziko hayo, haraka atarejea nchini na kuanza mikakati ya kukiandaa kikosi chake kwa ajili ya mwendelezo wa Ligi Kuu Bara ambapo mechi yao ya kwanza itakuwa ugenini dhidi ya Mbao FC.
“Tupo mapumzikoni ndiyo maana nimeamua kurudi nyumbani kwa mapumziko, mara baada ya kumalizika kwa mapumziko haya nitarejea haraka kuendelea na maandalizi ya mechi za ligi,” alisema Lwandamina.
Yanga wapo nafasi ya tatu kwenye Ligi Kuu Bara wakiwa na pointi 21 na taarifa zinasema kuwa kocha huyo ameondoka akiwa amekabidhi majina ya wachezaji ambao watasajiliwa kwenye dirisha hili.
Tupe Maoni Yako