SUALA la fungu lililobaki la usajili wa straika wa Yanga, Obrey Chirwa, limechukua sura mpya baada ya kigogo mmoja wa klabu hiyo kuamua kuachia ngazi, huku baadhi wakidai kuwa kigogo huyo ameamua kufanya hivyo kuepuka lawama.
Chirwa ambaye aliripotiwa kuomba ruhusa ya kwenda kwao Zambia kwa ajili ya matatizo yake ya kifamilia, lakini baadaye ilidaiwa amegoma kurejea Jangwani, akiwashinikiza mabosi wa Yanga kummalizia fedha zake za usajili.
Imedaiwa kuwa sababu ya straika huyo ‘kususa’ kurejea nchini ni kutokana na mvutano kati ya mchezaji huyo na uongozi wa klabu ambao unadaiwa kushindwa kummalizia fungu lililobaki kutokana na baadhi ya wajanja wachache kugawana kinyemela.
Habari zinasema wakati nyota huyo anasajiliwa mwaka 2016, tayari alishatengewa Dola 100,000 (zaidi ya Sh milioni 200 za Tanzania), lakini sehemu ya fedha hizo zilichotwa na wapiga dili.
Ni kutokana na mkanganyiko huo, inaelezwa kwamba tayari kigogo mmoja wa Yanga ameandika barua ya kuuacha wadhifa wake, sababu ikitajwa kuwa ni baada ya baadhi ya watu kumshutumu kuhusika na sakata la Chirwa.
DIMBA lilimtafuta Katibu Mkuu wa klabu hiyo, Charles Boniface ‘Mkwasa’, ili kuthibitisha suala hilo lakini akasema hana taarifa hizo, japo taarifa kutoka Yanga zinadai kuwa ni kweli yupo kigogo aliyeamua kuachia ngazi.
“Siwezi kuthibitisha juu ya suala hilo kwa kuwa sijapata barua yoyote kutoka kwa kiongozi yeyote kujiuzulu na mimi juzi nilikuwa ofisini mpaka usiku,” alisema Mkwasa.
Akizungumzia kuhusu tetesi hizo za baadhi ya wajanja kumega fedha za Chirwa, Mkwasa alisema hana uhakika ila anachojua yeye ni kwamba mchezaji huyo ana madai yake na wanafanya taratibu za kumlipa.
Alipoulizwa juu ya ujio wa mchezaji huyo, Mkwasa alisema tayari yupo nchini tangu juzi usiku na sasa wanafanya jitihada za kumaliza tatizo lake ili aweze kujiunga na wenzake kwa ajili ya maandalizi ya michuano mbalimbali.
Kwa mujibu wa habari za ndani, Yanga walikuwa wanahaha kuhakikisha kuwa mchezaji huyo anarejea nchini, baada ya kumwambia kuwa madai yake yote yataisha baada ya yeye kuwasili nchini.
Taarifa zaidi kutoka Yanga zinadai kuwa mzigo mkubwa kwa sasa umemwelemea Mkwasa kwani anafanya kila linalowezekana kuhakikisha wachezaji wanalipwa mishahara yao huku ikidaiwa kuwa wapo wajanja wachache walioifanya klabu hiyo kuyumba.