MWENYEKITI wa Baraza la Wazee wa Yanga, Ibrahim Akilimali amemtetea mshambuliaji wa kimataifa wa Yanga, Mzambia, Obrey Chirwa kufuatia kukosa penalti katika mechi ya juzi dhidi ya URA ya Uganda kwenye Kombe la Mapinduzi.
Yanga iliondolewa katika nusu fainali kwa penalti 5-4 ambapo Chirwa alikosa kwa upande wa Yanga na kusababisha kuwa gumzo kutokana na tukio hilo.
Akizungumza na Championi Ijumaa, Akilimali alisema Chirwa hakufanya makosa katika kupiga penalti ya mwisho kwani alidhamiria kufunga na kilichotokea ni bahati mbaya na kudai kuwa, kocha ndiye anayepaswa kulaumiwa kutokana na kumtumia licha ya kutokuwa na mazoezi ya pamoja na wenzake.
“Yanga tumetolewa kiume katika michuano ya Mapinduzi kwani hadi tunatoka tumefanikiwa kufanya vyema hadi dakika 90 lakini kilichotokea hakipaswi kulaumiwa mchezaji.
“Timu ilicheza vizuri ilipambana na hatimaye kuweza kufikia hapo tulipofikia na ilikuwa ni lazima timu moja isonge mbele.
“Siwezi kumlaumu Chirwa, kilichotokea ni bahati mbaya kwani, hata wachezaji wazuri Ulaya wanakosa penalti sembuse yeye, anayepaswa kulaumiwa ni kocha kwanini amemchezesha mchezaji akiwa hana mazoezi, naona anayarudia yaleyale ya Kocha Hans Pluijm,” alisema Akilimali.
Tupe Maoni Yako