Friday, December 8, 2017

Mawingu Tz

TETESI:Jamal Mnyate Kuitosa Simba...Kumalizana Na Lipuli MUda Wowote

KLABU ya soka ya Lipuli ya mkoani Iringa, ipo mbioni kumalizana na winga wa Simba, Jamal Mnyate, ili kuimarisha kikosi chao kabla ya kufungwa kwa usajili wa dirisha dogo Desemba 15, mwaka huu.
Mnyate amekuwa chaguo la makocha wazawa wa Lipuli, Amri Said na Selemani Matola, tangu kumalizika kwa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu uliopita, lakini Simba hawakuwa tayari kumwachia licha ya winga huyo kusugua benchi.
Akizungumza na Chandimu  jana, Amri ambaye ni kocha mkuu wa timu hiyo, alisema Mnyate alikuwa na mazungumzo na uongozi wa klabu hiyo hivyo mbichi na mbivu zitajulikana leo ikiwa atakubali kusaini mkataba au vinginevyo.
“Mnyate anaendelea kufanya mazungumzo na uongozi ambao ndilo jukumu lao, wametupa taarifa kuwa hadi kufika kesho (leo) watakuwa wamemalizana, kwa sababu mchezaji mwenyewe ameonyesha nia ya kutaka kujiunga na kikosi chetu,” alisema.
Amri aliongeza kuwa wachezaji wengine watawasili leo kuendelea na mazungumzo, lakini hakuwa tayari kutaja majina akihofia kuzungukwa na timu nyingine.
Alisema ripoti ambayo iliwasilishwa na benchi la ufundi kwa viongozi wa klabu hiyo inajumuisha wachezaji waliotakiwa ili kuboresha kikosi na sita watakaoachwa.

Tupe Maoni Yako