Kung’olewa kwa Simba katika michuano ya Kombe la Mapunduzi baada ya kuchapwa bao 1-0, kumezua mjadala mpya kuhusiana na Kocha Joseph Omog.
Omog raia wa Cameroon, alifungashiwa virago vyake na uongozi wa Simba ambao ulitumia maneno matamu kusema wamekubaliana aondoke baada ya kuvuliwa ubingwa wa Kombe la Shirikisho na Green Worries inayoshiriki ligi daraja la pili. Lakini baada ya kipigo cha leo, mashabiki wameanza kuhoji kama ilikuwa sahihi kumuondoa Omog.
Baadhi ya mashabiki wa Simba na wa timu nyingine wameeleza kuwa Simba ilikurupuka kumuondoa kocha huyo. Lakini wako waliosema tatizo kubwa ni wachezaji wenyewe ambao wameshindwa kujituma na kuonyesha wanataka kushinda.
Pia kuna mashabiki ambao wameelekeza lawama zao moja kwa moja kwa Kocha Irambona Masoud Djuma kwamba mfumo wake unaonekana kuwa mgumu na si imara katika ulinzi.
Kipigo hicho leo kwenye Uwanja wa Amaan mjini Zanzibar kimekuwa cha pili mfululizo kwa Simba. Mechi iliyopita, Simba ilikutana na kipigo kama hicho kutoka kwa Azam FC na matumaini yao kuendelea ilikuwa leo dhidi ya URA. Bao la URA lilipatikana dakika za nyongeza za kipindi cha kwanza na kipindi chote cha pili, Simba ilishindwa kupata angalau bao moja.
Tupe Maoni Yako