Tuesday, January 2, 2018

Mawingu Tz

Gadiel, Buswita Wakwama CAF


YANGA wamepeleka kikosi cha wachezaji 20 kwa Shirikisho la Soka Afrika (Caf), kitachoshiriki Ligi ya Mabingwa Afrika mwakani huku saba majina yakikwama.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Yanga, Dismas Ten, alisema hawajatuma majina ya wachezaji ambao hawakuwamo katika kikosi kilichopita.
Ten alisema mpaka jana mchana walikuwa wametuma majina ya wachezaji 20, lakini yakikosekana ya wale waliosajiliwa dirisha kubwa na dogo la msimu huu, wakiwamo makipa Ramadhan Kabwili na Youthe Rostand.
Wengine ni mabeki Gadiel Michael, Abdallah Shaibu na Feston Kayembe, kiungo mshambuliaji Pius Buswita na mshambuliaji Yohana Nkomola, lakini jina na Papy Tshishimbi likijumuishwa kwenye orodha iliyotumwa.
Tshishimbi ni miongoni mwa wachezaji wapya waliosajiliwa na Yanga katika dirisha kubwa la Ligi Kuu Tanzania Bara lililofungwa Agosti 6, mwaka huu.
Hata hivyo, alisema walishindwa kuwajumuisha wachezaji 27 katika orodha iliyopelekwa Caf kutokana na changamoto ya mtandao.
Ten alisema wanatarajia kuwaongeza wachezaji hao baada ya mtandao kutengamaa, ambapo mwisho wa kutuma usajili Caf ni kesho.
“Tulikuwa na changamoto ya mtandao ambayo imesababisha kutowajumuisha wachezaji saba, lakini jina la Juma Mahadh tumeliondoa katika orodha ya wachezaji tutakaowatumia katika mashindano ya kimataifa,” alisema.
Alisema mipango yao ni kufika mbali katika mashindano ya mwakani.
Katika hatua nyingine, alisema kuwa mshambuliaji wao, Obrey Chirwa, anatarajia kurejea leo akitokea kwao Zambia.
Ten alisema mshambuliaji huyo anatarajiwa kuungana na wenzake visiwani Zanzibar watakaoshiriki michuano ya Kombe la Mapinduzi.

Tupe Maoni Yako