Tuesday, December 19, 2017

Mawingu Tz

Yanga Yaigomea Simba

BENCHI la Ufundi la Yanga limefurahishwa na kurejea uwanjani kwa straika wao, Amissi Tambwe, lakini mabosi wa Jangwani wamepokea kwa mshtuko taarifa ya kuongezwa muda wa kufungwa dirisha dogo la usajili, kisha kwa kauli moja wakatamka kuwa hii ni janja ya mabosi wa soka nchini kuwabeba watani zao, Simba.
Mabosi hao wameshika vichwa kwa masikitiko na kusisitiza wao hawataongeza mchezaji yeyote licha ya Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF) kuongeza muda wa usajili mpaka wikiendi hii kwa madai ya mfumo wa usajili wa njia ya elektroniki (TMS) kuzingua kabla dirisha la usajili halijafunguwa Ijumaa.
Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Yanga, Hussein Nyika, aliliambia Mwanaspoti jana jioni kuwa kutokana na muda kuwa mchache hawataweza kufanya usajili wowote zaidi ya nyota wawili waliowasainisha mapema.
Nyota hao ni Mkongomani Fiston Kayembe na straika mzawa Yohana Mkomola, lakini bosi mwingine wa klabu hiyo aliyeombwa kuhifadhiwa jina, alisema kilichofanywa na TFF ni kuibeba Simba.
“Haiwezekani ishu hii iibuke ghafla, bila shaka ni mipango tu ya kuwabeba Simba hasa kuhusiana na sakata la beki waliyemchukua kutoka Lipuli (Asante Kwasi),” alisema kigogo huyo huku Nyika akisisitiza uamuzi wa TFF hauna afya ya kuwawezesha wao kufanya usajili tena na mambo yatabaki kama yalivyo.
Wakati Yanga wakiichunia ofa hiyo ya TFF, upande wa pili huenda ikawa ni faida kwa Simba kwani itawapa fursa nzuri ya kuweka mambo sawa katika suala zima la Kwasi aliyesajiliwa kutoka Lipuli hasa kwa kuwa timu hiyo ya Iringa imeendelea kumng’ang’ania mchezaji huyo.
Kwasi, usajili wake wa kutua Simba bado unakiza kizito kutokana na Lipuli kutangaza wachezaji iliowaacha huku jina la beki huyo likikosekana na imesisitiza kwamba bado ni mchezaji wao halali aliyebakiza miezi minane katika ajira yake.
Ongezeko hilo la muda wa usajili, sasa linaweza kuifanya Simba kuitafuta Lipuli na kukaa nao mezani katika kumaliza ubishi huo ingawa Mwanaspoti linafahamu kwamba wapo viongozi wa Serikali ya Mkoa wa Iringa wanaweka ngumu wakitaka kuona Lipuli inakomaa hadi mwisho .
Sakata la usajili huo linaelezwa kusababisha baadhi ya viongozi wa Lipuli kujikuta wakihojiwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).
Beki huyo ndiye mchezaji wa klabu hiyo aliyefunga mabao mengi katika Ligi Kuu Bara.

TAMBWE ARUDI
Nahodha wa Yanga, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ amesema kurejea kwa Tambwe kutawaimarisha katika mechi za Ligi Kuu Bara na zile za Ligi ya Mabingwa Afrika.

Tupe Maoni Yako