DIRISHA dogo la usajili likitarajiwa kufungwa Ijumaa hii, straika wa pembeni wa zamani wa Simba aliyekuwa Singida United, Pastory Athanas, ametua Kagera Sugar tayari kukinukisha katika mechi za Ligi Kuu Bara iliyosimama kwa muda.
Kagera imeamua kumsajili straika huyo anayeungana na nyota wa zamani wa Yanga, Ndanda na JKT Ruvu, Atupele Green ili kumaliza ukame wa mabao.
Wana Nkurukumbi wanaoshikilia nafasi ya 10 wakiwa na alama 11, wamefunga mabao saba tu katika mechi 11 za ligi hadi sasa, huku wakiruhusu mabao tisa jambo lililomfanya Kocha Mecky Maxime kuimarisha zaidi eneo hilo la mbele kurekebisha mambo.
Maxime alisema anaamini usajili aliofanya mpaka sasa kikosini, utatarejesha makali ya Kagera iliyomaliza msimu uliopita katika nafasi ya tatu kabla ya kuanza vibaya msimu hadi hivi karibuni ilipoanza kujitutumua.
Maxime alisema usajili wa wachezaji hao wawili ni wa mwisho kwa kikosi chao na sasa wanaingia kufanya maandalizi kwa mechi zao zijazo za kumalizia duru la kwanza kabla ya kujipanga upya kwa duru la pili litakaloanza mwakani.
“Tumemnasa Athanas (Pastory) ambaye tunaamini akishirikiana na Atupele na wengine waliopo kikosini wataisaidia timu kwa mechi zilizosalia,” alisema.
Tupe Maoni Yako