Kama unavyofahamu Kilimanjaro Stars imetupwa nje ya kombe la Chalenji huku ikiwa haijashinda hata mchezo mmoja kati ya minne iliyocheza kwenye kundi lake lililokuwa na timu tano. Tanzania ilipoteza mechi zake tatu (Tanzania bara 1-2 Zanzibar, Rwanda 2-1 Tanzania bara, Kenya 1-0 Tanzania bara) na kutoka suluhu katika mechi moja (Libya 0-0 Tanzania bara).
Kocha mzoefu Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ ambaye kwa sasa anafundisha Dodoma FC inayoshiriki ligi daraja la kwanza matokeo waliyopata Kili Stars kama wangepata vijana wa Serengeti Boys ‘sasa Ngorogoro Heroes’ waliocheza AFCON U17 hakuna mtu ambaye angeshangaa kwa sababu tungesema tunawapa uzoefu vijana.
Julio pia amegusia suala la kocha Ammy Ninje kupewa timu, kwa upande wake amesema, hana tatizo na kocha huyo isipokuwa inawezekana hana uzoefu wa kutosha kufundisha timu ya taifa ukizingatia amekaa nje ya nchi kwa muda mrefu hivyo inawezekana anakosa uzoefu kwa wachezaji wa kibongo na tamauni zao.
“Mimi simpingi Ammy ni kijana wangu na alikuja kucheza kwenye timu ya taifa, lakini kwa jinsi alivyoishi huko hatujui kazi yake kubwa aliyokuwa anafanya ingawa inasemekana ni kocha wa vijana lakini tusiamini kila mtu kwa kipindi hiki tulichonacho. Wachezaji wetu wanahitaji kumzoea mtu kulingana na mazingira, anaweza kuja mtu akawa na style yake halafu wachezaji wakashindwa kwenda nayo kwa kipindi hicho kifupi cha mashindano.”
“Lakini kama suala la muungano si yupo Mecky Maxime ambaye ndio alikuwa kocha bora, unapokuwa kocha bora maana yake nini? Unapokuwa kocha bora inawezekanaje usiwe kocha wa timu ya taifa. Uongozi wa TFF uliopita ulikuwa na ukiritimba na chuki ya kukataa watu fulani kwa sababu ya faida zao sasa hivi naona TFF ina watu ambao tunategemea wanabusara na ueledi mkubwa watu kama Kidao amecheza mpira sasa hivi ni Kaimu Katibu wa TFF, Msafiri Mgoyi ni muumini wa timu za vijana.”
“Nilitarajia matokeo haya tungeyapata kwa timu yetu ya Serengeti Boys kwa sababu tungekuwa tunatengeneza exposure kwa vijana lakini tunapeleka timu hiyohiyo wachezaji ambao kila siku tunafungwa. Tungepeleka watoto tungesema tunawapa uzoefu lakini tumepeleka wakubwa ambao ndio tunawategemea kwenye mashindano yote lakini bado tumefungwa.”
“TFF waangalie kwa umakini mkubwa sio tunaaminia tu kwa sababu ambazo wanazijua wao mwisho wa siku Ammy anarudi Uingereza aibu inakuja kwetu. Tatizo halianguki kwa Ammy inaonekana TFF wakosefu hakuna makocha wa kufanya kazi.”
Kuna wakati Julio na Charles Boniface Mkwasa walikuwa makocha wa timu ya taifa, lakini jambo ambalo si la kutegemewa wachezaji wao waliwahi kuzomewa na mashabiki kutokana na matokeo mabovu, Julio ametoa ufafanuzi juu ya hilo.
“Mimi nimefundisha Simba, Mkwasa amefundisha Yanga kwa bhiyo tunapokuwa na wachezaji wa Yanga watatu, Simba saba kwa sababu yupo Julio, wachezaji wa Simba watazomewa lakini wakiwa wa Yanga tisa wa Simba watatu wa Yanga watazomewa. Hatuwezi kufika, na wapenzi wa soka ndio tunasababisha hali hii, turudi kwenye wakati ule aliokuwepo Marcio Maximo wakati timu inahamasishwa na na aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Jakaya Kikwete.”
“Rais Kikwete alikuwa analipa makocha na aliupenda mpira kwa kiasi kikubwa, kama tungempa support kubwa leo tungfekuwa mbali sana kwenye soka lakini mchango wote wa Kikwete umepotelea hewani bila kujijua matokeo yake leo tunahangaika.”
“Ninaimani TFF mpya iliyoingia kama wanataka kumpa timu kocha mzawa kama vile Mayanga basi apewe stahiki zote zinazostahili ambazo angepata kocha mzungu lakini ukimnyima inakuwa tatizo na wapenzi nao wai-support timu yao ya taifabila kujali huyu Yanga wala Simba maana ndio siasa za mpira wan chi hii kinyume cha hapo hatuwezi kupata mafanikio ndio maana unaona timu yetu inaenda hovyo.”
“Wachezaji wetu lazima wajitoe bila kujitoa hatuwezi kupata mafanikio, angalia Zanzibar siku zote tukicheza nao, mimi nikiwa mchezaji wa timu ya taifa tumecheza na Zanzibar mara mbili, moja Uganda wakawa mabingwa marea ya pili Malawi zote walitufunga goli mojamoja kwa sababu wachezaji wa kizanzibar wana commitment wanapotaka kushindana matokeo yake leo wanaonekana wanatumia dawa za kusisimua misuli. Kwa hiyo tujifunze kutoka kwao.”
Hatua ya makundi ya Challenge Cup imehitimishwa jana jioni ambapo tayari timu nne zilizofuzu hatua ya nusu fainali zimeshajulikana na zilizoaga mashindano tayari zinafahamika. Zanzibar walipoteza mechi yao kwa kufungwa 1-0 na Libya lakini wamefanikiwa kupenya kucheza nusu fainali ambapo watacheza dhidi ya Uganda (mabingwa watetezi) siku ya Ijumaa.
Tupe Maoni Yako