KLABU ya Wekundu wa Msimbazi Simba, imejiwekea tahadhari baada ya kukumbuka jinsi walivyokuwa wakipigwa bao pale walipokuwa wakiweka bayana majina ya wachezaji wanaotaka kuwasajili na sasa wameamua kufanya mambo yao kimyakimya.
Awali Simba walikuwa na mipango ya kumsajili Mkongo Walter Bwalya, lakini ghafla Azam wakazunguka mlango wa nyuma na kufanya naye mazungumzo na sasa Wekundu hao wameamua kuficha usajili wao.
Akizungumza nasi jana, kocha msaidizi wa kikosi hicho, Massoud Djuma, alisema wapo mbioni kusajili wachezaji watatu hadi wane, lakini wanaelekeza nguvu zaidi kwa wazawa, huku akificha majina yao.
“Tunaendelea na mchakato wa usajili na tunahitaji wachezaji watatu hadi wane, ikiwa ni mchezaji mmoja kutoka katika kila safu kwenye timu, pia tunapendekeza zaidi wachezaji wa ndani lakini kama tutakosa kabisa ndipo tutageukia nje ya nchi,” alisema.
Kocha huyo aliyejiunga na Simba hivi karibuni akitokea Rayon Sport ya Rwanda, baada ya mechi yao na Lipuli FC iliyopigwa wiki moja iliyopita jijini Dar es Salaam na kutoka sare ya kufungana bao 1-1, alisema Simba inahitaji kufanya marekebisho kwenye nafasi za beki wa kati, mshambuliaji mmoja na kipa.
Alisema licha ya kuwa wamefanya usajili mzuri kwa ajili ya msimu mpya, lakini bado inahitaji kufanya marekebisho kwa ajili ya ligi na michuano ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho barani Afrika mwakani.
Tupe Maoni Yako