Monday, December 4, 2017

Mawingu Tz

TETESI Mpya Za Usajili Kutoka Simba Na Yanga Leo Jumatatu dec 4 2017..Unaambiwa Mastraika Hatari Kutua

SIMBA na Yanga hazijafanya usajili mkubwa mpaka sasa, lakini tayari mabosi wao wana majina matano ambayo hadi kufungwa kwa usajili wa dirisha dogo Januari 15 mambo yatakuwa mazuri.
Yanga iliyoko chini ya kocha Mzambia, George Lwandamina tayari imewapa mikataba beki Mkongomani, Fiston Kayembe na straika kinda, Yohana Mkomola lakini bado inasaka nyota wa maana hasa wa eneo la ushambuliaji. Ukiachana na mastraika watatu wa kigeni ambao watakuja kwa majaribio Yanga, klabu hiyo imeweka pia akili zake kwa nyota watano wazawa ambao wanapatikana kirahisi. Wageni hao ni Bensua Da Silva, Badara Kella na Adam Ziriku, ambaye inadaiwa tayari amejiunga na Zesco United.
Simba ya Mkameruni, Joseph Omog licha ya kutofanya usajili, nayo inachuja kuona imchukue nani kati ya nyota hao watano wazawa. Nyota ambao wanatajwa kuwindwa na Simba na Yanga ni Hassan Kabunda wa Mwadui, Mohammed Rashid Tanzania Prisons, Hamis Abdallah anayecheza Sony Sugar ya Kenya na Elias Maguli aliyeachana na Dhofar FC ya Oman.
Mwingine ni Habib Kiyombo wa Mbao FC, ambaye msimu huu amepachika mabao matano msimu huu. Kwa upande wake Hamis Abdallah alisema; “Nimeongea na viongozi wa Yanga, hasa Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili, Husein Nyika na aliniambia kama mipango yao itakwenda sawa wanaweza kunifata kokote nilipo na kunisainisha.”
Yanga inamtaka Hamis ili kuimarisha safu yake ya kiungo kutokana na Mzimbabwe, Thaban Kamusoko kukumbwa na majeraha ya mara kwa mara.
Kabunda tayari amekiri kuwa kwenye nafasi nzuri ya kutua Simba na anachosubiri ni viongozi hao wa Msimbazi kumalizana na timu yake kwani, tayari wamekubaliana maslahi binafsi. Simba inamhitaji aje kusaidiana na Shiza Kichuya katika winga zake.
Simba na Yanga zote zimeweka nguvu kuimarisha safu zake za ushambuliaji, ambapo Rashid aliyeifungia Prisons mabao sita mpaka sasa Ligi Kuu na Kayombo aliyeifungia Mbao matano, wanaonekana kuwa chaguo sahihi. Nyota hao tayari wamekiri kuwa kwenye mazungumzo na klabu hizo, na kama mambo yatakwenda vizuri, huenda wakasaini.
OMOG, MKWASA ANENA
Omog alisema ameshakabidhi ripoti yake kwa kamati ya usajili na ametaja aina ya wachezaji anaowahitaji. “Tuna michuano mingi msimu huu, hivyo nahitaji kuwa na kikosi kipana na wachezaji wenye uwezo sawa na katika ripoti yangu nimesisitiza hilo,” alisema Omog.
Kwa upande wa Katibu Mkuu wa Yanga, Charles Mkwasa alisema; “Tutasajili kutokana na mapungufu yaliyokuwa katika kikosi chetu kwani, mzunguko huu wa kwanza tulikuwa na majeruhi wengi ambao walichangia kutokufanya vizuri zaidi. Kila kitu kinakwenda vizuri ni suala la utekelezaji tu”

Tupe Maoni Yako