Saturday, December 16, 2017

Mawingu Tz

Simba, Yanga Zang’atwa Sikio Kimataifa


TIMU za Simba na Yanga zimeng’atwa sikio, baada ya kutakiwa kujipanga zaidi ili ziweze kufanya vizuri katika michuano ya kimataifa ya Afrika itakayoanza mwakani.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Shirikisho la Soka Afrika (Caf) juzi, Yanga wataanzia nyumbani kwa kucheza na St. Louis ya Shelisheli katika mchezo wa awali wa Ligi ya Mabingwa Afrika.
Simba ambao ni mabingwa watetezi wa Kombe la Azam (ASFC), nao wataanzia nyumbani kwa kucheza na Gendarmerie Tnale ya Djibouti katika mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika.
Wakizungumzia ratiba ya michuano hiyo, kocha wa zamani wa Yanga, Kenedy Mwaisabula, alisema timu hizo zinatakiwa kujipanga kikamilifu ili ziweze kuiwakilisha vizuri nchi.
Mwaisabula alisema timu hizo zinatakiwa kufanya maandalizi ya uhakika kwa kuwa michuano iliyo mbele yao ni migumu.
“Ule mzaha unaofanywa kila mwaka na timu za Tanzania katika maandalizi ya kimataifa ufike kikomo, kwani lazima Simba na Yanga zijue zina majukumu gani kwa Watanzania ili waweze kuyatimiza kikamilifu.
“Uongozi wa timu hizo hauna budi kuhakikisha wanatimiza yale yanayohitajika kwenye mabenchi yao ya ufundi, kwa kuwa mafanikio ni maandalizi,” alisema Mwaisabula.
Kwa upande wa mshambuliaji wa zamani wa Yanga, Mohamed Hussein ‘Mmachinga’, alisema Simba na Yanga hazitakiwi kuzidharau timu watakazoanza kucheza nazo, licha ya kuonekana ni nyepesi.

Tupe Maoni Yako