Tuesday, December 12, 2017

Mawingu Tz

Mastaa Yanga Wamepania Kinoma Safari Hii, Mtakoma


SIMBA ndio inayoongoza msimamo wa Ligi Kuu Bara ikiwaacha watani zao Yanga kwa pointi mbili, lakini hilo halijawazuia vijana wa Jangwani kuwapiga vijembe vinara hao kwa kudai wajiandae kisaikolojia kushuka kileleni.
Simba inaongoza kwa pointi 23, huku Yanga ikiwa nazo 21 jambo linalowapa jeuri nyota hao wa Yanga kutamka kuwa Simba isianze kuhesabu ubingwa kwa sasa kwani ligi bado mbichi kabisa.Straika wa pembeni, Emmanuel Martin, alisema kwa jinsi ligi ya msimu huu ilivyo ngumu na ushindani mkubwa, ni wazi Simba isitarajie ubingwa kwa sasa.
“Akili yetu kwa sasa ni kuona tunarejea kwenye ligi ili kuhakikisha tunafuta pengo la pointi na kuweka letu ili kutetea ubingwa, wanaodhani ubingwa upo mikononi mwao itakula kwao, ligi bado mbichi,” alisema Martin aliyesajiliwa Yanga akitokea JKU.
Naye beki wa kati ya timu hiyo, Andrew Vicent ‘Dante’ alisema Simba kuwa kileleni hakuwanyimi usingizi, ila anawatumia salamu kwamba wasichonge sana ligi itakapoanza watawatoa kileleni.
“Tuna mahesabu yetu, hatugombanii pointi na wao, sisi kazi yetu ni hesabu za ubingwa, tunajua tunacheza na Mbao ambayo ina ushindani, lakini tunaamini tutawafunga na tutazidi kusonga mbele,” alisema Dante.
Naye kipa Beno Kakolanya ambaye amekuwa katika sintofahamu na mabosi wake kushinikiza kulipwa fedha zake za usajili, alisema kama wenzake Jangwani wataamua watapindua matokeo na kurejea kileleni na mwishowe kutetea taji.
“Yanga ipo makini kwa mahesabu ya ubingwa na rekodi hazidanganyi kwani kuna wakati Simba ilikuwa mbele kwa zaidi ya pointi 11, lakini tulizipunguza hadi kuwa mbili na hatimaye tukaibuka kuwa mabingwa,” alisema Kakolanya.
“Kikubwa ni sisi kuendelea kujipanga ili kuhakikisha tunashinda kila mechi inayokuja mbele yetu, uwezo huo Yanga inao.”
-Mwanaspoti

Tupe Maoni Yako