Saturday, December 9, 2017

Mawingu Tz

Mambo 10 Usiyoyajua Kuhusu Sergio Ramos


JINA la Sergio Ramos si geni masikioni mwa mashabiki wa soka, hasa wa La Liga. Mbali na sifa nyingine ikiwamo uwezo wake wa kutupia mabao, nahodha huyo wa Real Madrid anawavutia wengi kutokana na aina yake ya uchezaji wa kujitoa anapokuwa uwanjani.
Hivi karibuni, wakati kikosi chake kikiumana na Athletic Bilbao, Ramos aliweka rekodi ya kuwa mchezaji mwenye kadi nyekundu nyingi La Liga (19), akiwazidi wakongwe, Pablo Alfaro na Xavi Aguado, waliokuwa wamekutana na adhabu hiyo mara 18 kila mmoja.
Je, ukiachana na hilo, uliyajua haya kuhusu nyota huyo ambaye pia ni nahodha wa timu ya Taifa ya Hispania?
  1. Ramos mwenye umri wa miaka 30, ni mume wa mwandishi wa habari maarufu wa Hispania, Pilar Rubio, ambaye amezaa naye watoto wawili; Sergio na Marco. Wawili hao walianza kuripotiwa kuwa na uhusiano wa kimapenzi mwaka 2012.
  2. Akiwa na umri wa miaka 19, Ramos aliitwa kwa mara ya kwanza kwenye kikosi cha timu ya Taifa ya Hispania. Hivyo, alivunja rekodi iliyodumu kwa miaka 55 ya kuwa mchezaji mwenye umri mdogo kutinga ‘uzi’ wa kikosi hicho.
  3. Wakala wake ni Rene Ramos, ambaye ni kaka yake. Jamaa huyo ndiye aliyesimamia dili la Ramos kutua Madrid akitokea Sevilla mwaka 2005, akiwa ndiye chipukizi wa kwanza wa Hispania kununuliwa kwa ada kubwa (euro milioni 27).
  4. 4. Kutokana na ustadi wake wa kuwazuia washambuliaji, moja kati ya rekodi zake kali katika soka la Hispania ni kushinda tuzo ya Beki Bora wa La Liga kwa misimu minne mfululizo, yaani kuanzia mwaka 2012 hadi 2015.
  5. Baba yake mzazi, Jose Maria, ni shabiki mkubwa wa Manchester United. Ramos alifichua siri hiyo mwaka 2013, siku chache kabla ya Mashetani Wekundu hao kuvaana na Madrid katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya.
  6. Kabla ya kukutana na bibiye Pilar, Ramos alikuwa mmoja kati ya mastaa waliokuwa wakisifika kwa kujiachia na warembo. Aliwahi kutajwa kutoka na walimbwende, Lara Alvarez, Amaia Salamanca, Elisabeth Reyes, Nereida Gallardo na Carolina Martinez.
  7. Rafiki mkubwa wa Ramos ni kiungo wa Arsenal, Mesut Ozil, ambaye alicheza naye kwa misimu kadhaa Santiago Bernabeu. Ramos ni miongoni mwa wachezaji wa Madrid ambao hawakutaka Mjerumani huyo aondoke Hispania na kuhamia Arsenal.
  8. Mama mzazi wa Romas, Paqui, ni shabiki mkubwa wa Real Madrid na inasemekana huchangia kwa kiasi kikubwa uamuzi wa mwanawe huyo kukataa mara kwa mara ofa za kujiunga na klabuni nyingine ambazo zimekuwa zikimtaka.
  9. Ramos husherehekea ‘birthday’ yake Machi 30 kila mwaka. Kwa wafuatiliaji wa tasnia ya burudani, watagundua kuwa ni sawa na mwanamama anayefanya vizuri kwenye soko la muziki nchini Marekani, Celine Dion.
  10. Kwa upande wa mkwanja, beki huyo wa kati, ambaye pia anacheza vizuri eneo la mlinzi wa pembeni, anatajwa kumiliki utajiri wa Dola za Marekani milioni 60, zaidi ya Sh bil. 130 za Tanzania.

Tupe Maoni Yako