Friday, December 8, 2017

Mawingu Tz

Dili la Simba, kumbe Yanga wanahusika


YANGA imethibitisha ipo tayari kuanza mchakato wa kubadili mfumo wa uendeshaji klabu hiyo kuingia katika uwekezaji kama walivyofanya watani wao Simba waliomaliza biashara mwishoni mwa wiki iliyopita.
Lakini kama hujui, ni kwamba dili zima la bilionea Mohammed ‘MO’ Dewji kupewa timu na wanachama wa Simba, Yanga wanahusika bwana.
MO Dewji amepewa Simba kwa hisa za asilimia 50 zenye thamani ya Sh20 Bilioni japo mchakato unaendelea ili utambuliwe rasmi na bilionea huyo kuigeuza Simba kuwa moja ya klabu tajiri inayoendeshwa kisasa.
Hata hivyo serikali imekuwa ikisisitiza kuwa inataka kuona klabu zinatoa hisa kwa asilimia 49 na zinazosalia zinabaki kwa wanachama, mfumo ambao hata Yanga imedaiwa ndio inaoupigia hesabu.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati iliyoendesha zoezi la mabadiliko ya Simba, Mulamu Nghambi aliliambia gazeti hili, licha ya wanachama na mashabiki wa Wekundu wa Msimbazi kukenua kutokana na mabadiliko yaliyofanywa, lakini ukweli Yanga wanahusika kwa kiasi kikubwa kuwapa akili ya kufanikisha hilo.
Mulamu alisema Yanga ndio walifanya zoezi la mabadiliko ya mfumo wa kumpa dili MO kama mwekezaji ili iwe rahisi kutokana na kusoma mchakato wao waliouanza mapema miaka mingi iliyopita na kubaini kilichowakwamisha.
MSIKIE MWENYEWE
“Kikubwa kinachofurahisha kwa mchakato huu kukamilika ni kwamba tumeonyesha kumbe inawezekana klabu zetu kufanya mabadiliko na kuachana na mifumo ya kizamani tofauti na ilivyokuwa ikifikiriwa,” alisema.
“Kwa mwenye kumbukumbu nzuri atakubaliana na mimi kwamba suala kama hili, Yanga ndio wangekuwa wa kwanza kulifanya kwa sababu walishajaribu kama mara tatu au nne hivi lakini wakashindwa kulitimiza ikiwemo mara ya mwisho walijaribu mwaka 2007 kama sikosei.
“Kikubwa ambacho sisi tulikifanya ni kufanya utafiti wa kujua wapi Yanga ilikuwa imekosea na ilipoishia kiasi cha kuwakwamisha mchakato wao, kisa sisi tukaanzia hapo na kufanya mambo,” alisema Mulamu ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Soka Mkoa wa Dodoma (DOREFA).
YANGA WALIKOSEA WAPI?
“Baada ya utafiti wetu, tuligundua kwamba kikubwa ambacho wenzetu kiliwaangusha kwa kipindi hicho kilikuwa ni makundi mawili ambayo walikuwa nayo ambayo yalikuwa na mitazamo tofauti. Kundi la Yanga Asili na Yanga Kampuni hivyo tatizo likaja kwa nani ataisimamia timu ndipo wakavurugana,” alifichua zaidi.
Mulamu alisema Simba imefanya jambo la maana kwa kuingia kwenye mfumo huo na kumfanya MO kuwa mwekezaji namba moja kwa sababu ataisimamia timu kama mwanachama mwingine wa kawaida kutokana na mapenzi aliyonayo kwa klabu hiyo.
“Huyu MO ni mwenzetu na hata hili alilolifanya ni kwa sababu ana nia ya dhati ya kutaka kuona klabu hii inasonga mbele. Lakini pia mfumo huu unaisaidia hata serikali kupata mapato mengi kwani kila jambo litafanyika kwa mfumo unaoeleweka.”
-Mwanaspoti

Tupe Maoni Yako