SIKU chache baada ya mfanyabiashara Mohamed Dewji ‘Mo’ kutangazwa kuwa mshindi wa zabuni ya uwekezaji katika klabu ya Simba, tayari ameanza kuonyesha jeuri ya usajili kwa kumbakiza kiungo
Mohamed Ibrahim, ambaye alikuwa akifukuziwa kwa udi na uvumba na mahasimu wao, Yanga.
Mkataba wa miaka miwili wa mchezaji huyo aliyetokea Mtibwa Sugar, Mo Ibrahim, ulikuwa unatarajiwa kumalizika mwishoni mwa msimu huu, ambapo Simba walionekana kushindwa kutimiza masharti yake na Yanga kuanza mchakato wa kutaka saini yake.
Lakini baada ya taarifa za mchezaji huyo kukaribia kumwaga wino Yanga kupamba moto, Mo Dewji ameingilia kati suala hilo na kumalizana na Mo Ibrahim na leo atasaini mkataba mpya wa miaka miwili.
Taarifa za kuaminika zilizonaswa na Chandimu zinasema mazungumzo yamekamilika na Simba wako tayari kutimiza masharti ya mchezaji huyo, ambayo ni kuboreshewa maslahi yake, kupewa nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza na
kuruhusiwa kuondoka kama atapata timu nje ya nchi.
Chanzo cha ndani ya klabu ambacho hakikutaka jina lake litajwe, kimesema baada ya Mo Ibrahim kutoa masharti yake kupitia Meneja wake, Jamal Kisongo, Simba iliyaridhia na iko tayari kumwongeza mkataba nyota huyo.
“Baada ya Kisongo kuzungumza na mteja wake kukubaliana alifika ofisini kwetu kuwasilisha na tumekubaliana kumpa mkataba wa miaka miwili ambao atausaini kesho (leo),” kilisema chanzo hicho.
Chandimu Tulizungumza na Kisongo, ambaye alithibitisha kumalizana na uongozi wa Simba na mchezaji wake atasaini mkataba huo wa miaka miwili.
“Masharti yetu niliwapelekea Simba na hawakuwa na hiana na muda wowote kuanzia sasa ataongeza mkataba wa miaka miwili,”alisema Kisongo.
Wiki iliyopita, Mo Dewji alishinda zabuni hiyo baada ya kuweka mtaji wake wa Sh bilioni 20, sawa na asilimia 49 ya hisa, ambazo ni kwa agizo la serikali na kuachana na ule mpango wa wanachama wa kumpa mwekezaji huyo asilimia 50 kwa 50 na sasa ameanza jeuri ya usajili.
Tupe Maoni Yako