WAKATI benchi la ufundi la Simba likiweka wazi kuwa linahitaji kuongeza wachezaji ili kuimarisha kikosi hicho, beki wa zamani wa timu hiyo, Abdi Banda, ameelezea kushangazwa na uamuzi huo.
Simba ina mpango wa kusajili beki wa kati, mshambuliaji, winga na mlinda mlango, jambo ambalo beki huyo amedai kuwa haoni sababu ya kufanya hivyo wakati kuna wachezaji wanaosugua benchi.
Banda anayecheza soka la kulipwa nchini Afrika Kusini katika klabu ya Baroka FC inayoshiriki Ligi Kuu, alikiambia Chandimu kuwa, Simba hawana sababu ya kuhangaika kufanya usajili kutokana na kikosi kipana walichonacho.
“Usajili uliofanywa na Simba msimu huu unatosha kuwapa ubingwa na kufuta machungu ya kuukosa kwa misimu kadhaa iliyopita, lakini nashangaa kusikia benchi la ufundi linahitaji kuongeza wachezaji.
“Sasa wachezaji watakaosajiliwa watacheza wapi wakati wengine tayari wapo au ni lazima kusajili kila mwaka, au ndiyo biashara za watu wanahitaji kupata asilimia 10?” alihoji Banda.
Beki huyo alisema ufike wakati kwa timu kubwa hasa za hapa nchini kuwakubali wachezaji waliopo kikosini na kuwapa nafasi ya kucheza kwani waliwasajili wenyewe.
“Ujuaji na biashara zinazofanywa na viongozi ndani ya timu wakati wa usajili ndio vinachangia mchezaji kuonekana hana uwezo muda mfupi baada ya kusajiliwa.
“Kuna wachezaji tangu wasajiliwe na Simba wameishia kucheza mechi za kirafiki na kama wamepata nafasi ya kucheza Ligi Kuu Tanzania Bara, basi hazizidi mechi mbili na ukijiuliza walisajiliwa kwa kazi gani huwezi kupata jibu,” alisema.
Tupe Maoni Yako