Sunday, December 17, 2017

Mawingu Tz

Yanga Yawaachia Kazi Ajibu, Chirwa

Washambuliaji wa klabu ya Yanga, Ibrahim Ajibu na Obrey Chirwa ni kama wameendelea kuaminiwa na benchi la Ufundi la klabu hiyo, baada ya kuamua kutoongeza washambuliaji wengine.
Kabla ya kufunguliwa kwa dirisha hilo dogo la usajili Novemba 15, mwaka huu, Kamati ya Usajili ya Yanga chini ya Mwenyekiti, Hussein Nyika, ilipanga kuongeza wachezaji watatu kwenye nafasi ya ushambuliaji, beki na kiungo ili kuimarisha kikosi hicho.
Yanga ilitaka kuongeza mshambuliaji mwenye uwezo mkubwa kwa ajili ya kuwasaidia Ajibu na Chirwa ambao ndio walionekana kuibeba timu kwenye safu hiyo tangu kuanza kwa msimu huu.
Hata hivyo, mpaka dirisha linafungwa usiku wa kuamkia leo, Yanga haijasajili mshambuliaji wowote na sasa mikoba ya kuhakikisha wanapata mabao ya kutosha kwenye ligi na michuano ya kimataifa inaendelea kubaki mikononi mwa Ajibu, Chirwa na nyota waliotoka kwenye majeraha, Donald Ngoma na Amissi Tambwe.
Meneja wa timu hiyo, Hafidh Saleh, aliliambia Nipashe jana kuwa kocha Mzambia George Lwandamina, ameonyesha imani kubwa kwa Ajibu na Chirwa na kuamua kutosajili mshambuliaji mwingine.
“Usajili uliofanywa ni ule ule wa Nkomolwa (Yohana) na yule beki Mkongo Kayembe (Fiston), tutaendelea kuwategemea Chirwa na Ajibu lakini pia Ngoma (Donald) na Tambwe (Amissi) wamerejea,” alisema Saleh.
Alisema kwa sasa timu hiyo inaendelea na programu yake ya mazoezi na kesho itachea mchezo wa kirafiki dhidi ya Polisi Tanzania.
“Kocha aliomba mchezo wa kirafiki na Jumapili tutacheza dhidi ya Polisi Tanzania, lakini timu itakuwa chini ya makocha wasaidizi kwa sababu mwalimu Lwandamina ameomba ruhusa na ameenda kwao Zambia mara moja kwa ajili ya kuhuduria mahafali ya mtoto wake,” alisema Hafidh.

Hata hivyo, Yanga itakuwa na wakati mgumu kwenye ligi kama Ngoma na Tambwe hawatarejea kwenye viwango vyao na hivyo kocha Lwandamina kuwategemea zaidi Chirwa na Ajibu kitu ambacho kitaleta shida endapo mmoja atakuwa majeruhi.
Yanga inayodhaminiwa na Kampuni ya Kubashiri Matokeo Michezoni ya SportPesa, pia inajiandaa kwa ajili ya kushiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambayo imepangiwa kucheza na St Louis ya Shelisheli kwenye mchezo wa hatua ya awali utakaochezwa Februari mwakani.

Tupe Maoni Yako