Wednesday, December 6, 2017

Mawingu Tz

Utata Waibuka Kuhusu Asilimia Atakazopewa MO Baada Ya Kushinda Zabuni Simba

Baada ya mfanya biashara Mohammed Dewji MO kushinda zabuni ya uwekezaji ndani ya klabu ya Simba ambapo kutakuwa na mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji kutoka uanachama hadi hisa, mambo mengi yamekuwa yakizungumzwa kuhusu asilimia za hisa atakazopewa  tajiri huyo na zile ambazo zitabaki kwa wanachama.
Msajili wa vyama vya michezo Ibrahim Mkwawa ametoa ufafanuzi juu ya mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji kwa vilabu vilivyoanzishwa na wanachama kwenda kwenye mfumo wa hisa kama ilivyofanya klabu ya Simba.
Msajili huyo ameeleza kwamba, kanuni mpya za serikali zilizotoka mwezi October 2017 zinaeleza kwamba mfumo wa hisa ni asilimia 51 kwa 49.
“Kanuni hizi baada ya kutangazwa zimeshakuwa sheria na kwa mujibu wa kanuni hizi, kanuni ya 28 (a) (i) inasema kwamba, vilabu ambavyo vimeanzishwa na wanachamavikitaka kuuza hisa zake vinapaswa kutenga asilimia 51 kwa ajili ya wanachama wake na asilimia 49 kwa ajili ya mwekezaji. Kanuni ndio ziko hivyo, na kanuni kanuni hizo kabla ya mkutano mkuu zilipelekwa klabu ya Simba na wao wanazifahamu.”
“Kwa hiyo ni kitu ambacho kipo kwenye kanuni mabadiliko yake sasa hilo ni suala jingine lakini kwa sasa tunakwenda na 51 kwa 49.”
“Wao kama hawakuliweka wazi siku ya mkutano, mimi siwezi kulisemea walipaswa wawaambie wanachama wao lakini kimsingi walikuwa wanalifahamu.”
“Si dhani kama kutakuwa na mgongano kwa sababu ule ulikuwa utaratibu tu wa kumtangaza mshindi sio kwamba ndio amepewa hisa asilimia 50, kinachofuata sasa ni taratibu za kisheria ambazo moja kwa moja zitaangukia kwenye kanuni ambazo zimeshatungwa kwa hiyo hakuna mgongano wowote.”
“Wanachama na mashabiki wa mpira waelewe kwamba, serikali sasa imeshatunga kanuni ambazo itaziongoza klabu zote sio Simba tu, klabu zote za mpira wa miguu ambazo zinamilikiwa na wanachama kanuni sasa ziko tayari kama zinataka kwenda katika mfumo huu wa uendeshaji kwa njia za hisa, wazisome kanuni ambazo zimetungwa na serikali ambazo zinawataka wanachama wamiliki asilimia 51 na wawekezaji asilimia 49.”
Mitaani kumekuwa na mijadala mingi kuhusu asilimia za hisa kati ya MO na wanachama, wapo wanasema MO atamiliki 51% halafu wanachama watabaki na 49%, wapo wanaodai kila upande utakuwa na umiliki sawa yaani 50% kwa 50% lakini tayari serikali imeshaweka mambo sawa.

Tupe Maoni Yako