Monday, December 18, 2017

Mawingu Tz

Usajili wa Asante Kwasi Kwenda Simba Pasua Kichwa…

Jumapili ya December 17.2017 klabu ya Lipuli imeweka wazi majina ya wachezaji walioasajiliwa na walioachwa katika kikosi hicho cha Wanapaluhengo.
Katika orodha hiyo iliwekwa wazi na msemaji wa klabu hiyo, Clement Sanga walioachwa ni pamoja na:-
1:Wazir Ramadhani
2:Mussa Ngunda
3:Machaku Salum Machaku
4:Melvin Alistoto
5:Ahmed Manzi
6:Dotto Kayombo.
Hata hivyo orodha haijamjumuisha beki wa kati wa Zamani wa klabu za Mbabane Swallows na Mbao Fc Mgana, Asante Kwasi ambaye hivi karibuni ameripotiwa kusaini mktaba wa kuwatumikia mabingwa wa kombe la Shirikisho nchini Tanzania na vinara wa ligi kuu Tanzania bara, Simba sc.
Unaweza kusema usajili wake kwenda Simba ni Pasua kichwa kwani Usajili huo ulikumbwa na vikwazo ambavyo kwa namna moja ama nyingine vingeza kumzuia nyota huyo kujiunga na Wanamsimbazi hao.
Moja ya vikwazo vilivyoingilia ni pamoja na taarifa ambazo zimekuwa zikiuhusha mkataba wa Asante Kwasi kwa Lipuli kuwa na Kasoro.
Taarifa hizo za mkataba wenye kasoro ulivainishwa na gazeti la Bingwa toleo la tarehe 14.12.2017 ambalo lilieleza kuwa Kwasi huenda angesajiliwa Simba akiwa kama mchezaji huru. Taarifa hiyo ilisomela hivi:-
“Wakati zikiwa zimebaki siku chache kabla ya kufungwa kwa dirisha dogo la usajili, Simba watamnasa bure beki wa kati wa Lipuli, Asante Kwasi, licha ya mvutano uliojitokeza kati ya timu yake hiyo na Wekundu hao wa Msimbazi.
Licha ya mchezaji huyo kuichezea Lipuli katika mechi za mwanzo za Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu, lakini mkataba wake unadaiwa kuwa na dosari ambazo zitamrahisishia kutua kwa urahisi kwa Wekundu wa Msimbazi.
Suala la usajili wa mlinzi huyo linaonekana kuwachanganya viongozi wa Lipuli na kuwafanya wakutane kwa haraka kujadili, ambapo kwa siku nzima ya jana walikaa kikao wakilifanyia kazi.
Kwa mujibu wa taarifa ambazo BINGWA limetonywa kutoka chanzo cha uhakika ndani ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kuna uwezekano mkubwa Simba kumnasa mchezaji huyo bure (huru), kutokana na mkataba wake uliowasilishwa kwa shirikisho hilo kuonekana kuwa na kasoro.
Chanzo hicho kiliendelea kupasha kwamba, Simba itamchukua Kwasi kwa urahisi kwa kuwa hana mkataba na Lipuli, kwani awali alivyochukuliwa kutoka Mbao FC ya jijini Mwanza alipewa mkataba ulio na kasoro.
“Nakwambia Simba watamchukua Kwasi bure kwa sababu wanachokifanya Lipuli kwa sasa ni kumbana mchezaji wakati mkataba waliompa awali unaonekana una ukakasi kutokana na kuwapo kwa baadhi ya vipengele ambavyo havikuzingatiwa katika mkataba,” kilieleza chanzo hicho.
Wekundu hao wa Msimbazi wapo katika harakati za kumnasa beki huyo, licha ya usajili wake kuzua mvutano ndani ya uongozi wa Lipuli, ambao haupo tayari kumwachia aondoke kama mchezaji huru.
Awali kabla ya kuibuka utata huo, taarifa zilidai kuwa, iwapo Simba watamhitaji mlinzi huyo katika usajili wa dirisha dogo, basi watalazimika kuwatoa wachezaji wao, Juma Luizio na Jamali Mnyate, lakini sasa vinara hao wa Ligi Kuu Tanzania Bara wanaonekana watanasa saini ya beki huyo wa Ghana bila kuwatoa wachezaji wake.
Sakata hilo limefikia hatua hiyo kutokana na Simba kutaka kumsajili Kwasi kama mchezaji huru, baada ya kubaini dosari zilizopo kwenye mkataba, lakini Lipuli wanaweka ngumu katika suala hilo, wakidai mkataba wake haujamalizika.
Ili kujiridhisha juu ya mkataba wa mchezaji huyo na Lipuli, BINGWA liliwatafuta viongozi wa timu yake ya zamani, Mbao FC, aliyoichezea katika msimu uliopita wa Ligi Kuu Tanzania Bara, ili kupata ufafanuzi juu taarifa za usajili wake kutoka klabu ya Mbabane Swallows FC.
Akizungumzia suala hilo, Mwenyekiti wa klabu ya Mbao FC, Solly Njash, alisema walimsajili Kwasi akiwa mchezaji huru kutoka nchini kwao Ghana, ambapo walimsainisha mkataba wa mwaka mmoja alioutumikia msimu uliopita.
“Tulimsajili Kwasi kwa mkataba wa mwaka mmoja tu ambao aliutumikia na kuumaliza, lakini tulipotaka kumwongezea alikataa kwa madai kuwa kiasi cha fedha tulichotaka kumpa hakilingani na uwezo alionao, hivyo tukaachana naye,” alisema Njash.
Awali kabla ya mvutano huo kuanza, Kwasi aliwahi kulidokeza BINGWA kabla ya mechi za Ligi Kuu kusimama kuwa, ataondoka nchini kwenda kwao Ghana, lakini huenda asirejee katika kikosi cha Lipuli hadi atakapolipwa fedha anazodai.
Alisema kama watamlipa, basi atarejea kuendelea kuitumikia timu hiyo, lakini wasipotimiza sharti hilo hatarejea na badala yake ataangalia maisha katika timu nyingine zilizoonyesha nia ya kumhitaji.
Kwassi alizitaja timu zilizokuwa zikimhitaji kuwa ni Singida United, Simba na Yanga, huku akisisitiza kuwa, kikubwa ataangalia maslahi yake, kwani amekuja kufanya kazi ili apate fedha na si kufanya kazi bila kulipwa chochote.
Hadi gazeti linakwenda mtamboni, juhudi za kuwapata viongozi wa Lipuli ziligonga mwamba, kwani Katibu Mkuu, Wille Chikweo, kila alipopigiwa katika simu yake ya mkononi alipokea na kudai yupo katika kikao muhimu, hivyo apigiwe tena baadaye.”
Hata hivyo msemaji wa klabu ya Lipuli Fc, amesema Asante Kwasi bado ni mchezaji halali wa Lipuli na alisaini mkataba wa Mwaka mmoja ambao bado hajamaliza.
Kwa maelezo ya Sanga ameongeza kuwa mchezaji huyo atajiunga na Lipuli Muda wowote huku akiwa wataka Wadau na Wapenzi wa soka Kujitokeza kumpokea atakapo rejea kunako mji wa Iringa
Huyu Hapa Sanga Akitangaza Wachezaji Ambao wamesajiliwa na Walioachwa na Lipuli Dirisha Dogo.

Tupe Maoni Yako