Nahodha wa Yanga, Nadir Haroub 'Cannavaro' anaamini bado Yanga ina nafasi kubwa ya kutetea taji lake la ubingwa Ligi Kuu Bara kwa mara nyingine.
Cannavaro amesema Yanga hawajaanza vizuri msimu wao katika kile kiwango wanachotaka, lakini wana uwezo wa kurekebisha mambo.
"Bado tuna nafasi na ligi haiko mbali sana, umekuwa ukiona wachezaji wanavyojituma na si watu wa kuangalia matatizo au kulalamika tu.
"Mimi naona wachezaji wanastahili pongezi na wamekuwa wakionyesha juhudi kubwa sana. Hii inanipa moyo kuwa tukiendelea hivi, uongozi na wanachama na mashabiki wakawa nasi, tutafanya vizuri," alisema.
Yanga inarejea mazoezini leo na Cannavaro amekuwa kati ya wachezaji wanaoonyesha juhudi kubwa.
Nahodha huyo wa zamani wa Tanzania, Taifa Stars na Zanzibar Hereos, ni kati ya wachezaji waliocheza Yanga kwa muda mrefu na kuipatia mafanikio makubwa.
Baada ya mechi 11 za Ligi Kuu Bara, Yanga iko katika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 21 tofauti ya pointi mbili dhidi ya vinara Simba na Azam FC walio katika nafasi ya pili.
Tupe Maoni Yako