Thursday, December 14, 2017

Mawingu Tz

TFF watoa ufafanuzi, wachezaji Kili Stars kuvaa vivazi vya aibu

Shirikisho la soka nchini ‘TFF’ limetoa ufafanuzi baada ya wadau wa soka nchini kuonesha kukasirishwa na namna kikosi cha timu ya Tanzania Bara ‘Kilimanjaro Stars’ ilivyotawanyika wakati walipotua uwanja wa ndege wakitokea nchini Kenya waliposhiriki michuano ya ukanda wa Afrika Mashariki na Kati ‘CECAFA’.
Ikumbukwe kwamba baada ya kuwasili nchini, wachezaji wa Kilimanjaro Stars walionekana kuvaa mavazi yasiyokuwa ya sare lakini pia mavazi ambayo yaliwakasirisha wengi kutokana na kutokuwa na staha.
Akitoa ufafanuzi huo afisa habari wa TFF Alfred Lucas amesema mara baada ya kutua nchini walipanga kuwachukua wachezaji wote na kuwapeleka hotelini ambapo waliamini kabla ya kutawanyika wangepata nafasi ya kupumzika.
Amesema wazo hilo lilipingwa na baadhi ya wachezaji ambao walipendekeza kutokwenda hotelini na badala yake kuondoka na kuelekea majumbani, jambo ambalo lilikubaliwa na mkuu wa msafara na hivyo wachezaji wakaona ni vyema kubadilisha sare na kufaa nguo za kiraia.
Ilivyokuwa.
-Timu iliingia jana saa 2:30 asubuhi wakiwa katika sare za timu ya Taifa, walipofika pale tukawapa tangazo kuwa kambi imevunjwa kwa kuwa tayari wameshatolewa kwenye michuano ya CECAFA lakini tuliwaandalia siku moja ya kukaa hotelini, tulifanya maksudi ili wapate kupumzika, lakini baadhi yao wakasema hakuna haja ya sisi kwenda huko hotelini, Alfred amesema.
Alfred amesema kwa kuwa wengi walikuja pale wakiwa tayari wameshawasiliana na ndugu zao, wakaingia kwenye gari na kubadilisha sare za timu ya Taifa na kuvaa nguo za kawaida hivyo hawakujua kile ambacho wangekivaa kingewakera watanzania.
-Timu ya Taifa ina heshima ya kipekee kabisa bila kujali matokeo ya uwanjani kwa hiyo na ile heshima miongoni mwa nidhamu zake ni pamoja na kuvaa sare ili inapotokea kama timu ionekane na si kila mtu kuvaa mavazi yake, ameongeza.
Tanzania Bara ikishiriki katika michuano ya CECAFA ilishindwa kufanya vizuri baada ya kufungwa michezo mitatu na kutoka sare mchezo mmoja, matokeo ambayo yaliwafanya kumaliza wa mwisho katika kundi A na kuaga mashindano hayo mapema.

Tupe Maoni Yako