UONGOZI wa klabu ya Yanga jana ulikuwa kwenye hatua za mwisho za kumsainisha mshambuliaji wa Tanzania Prisons, Mohammed Rashid ‘Mo Rashid’ mkataba wa miaka miwili.
Mohammed Rashid ambaye anashika nafasi ya pili katika orodha ya vinara wa mabao, ambapo analingana na Obrey Chirwa wa Yanga, wote wakitingisha nyavu mara sita wakiwa nyuma ya mshambuliaji wa Simba, Emmanuel Okwi aliyefunga mara nane.
Meneja wa Mchezaji huyo, Samuel Sango, amethibitisha kwamba Yanga wanamhitaji mshambuliaji huyo ili kuongeza nguvu kwenye safu yao ya ushambuliaji, kutokana na mechi nyingi kuibuka na ushindi wa mabao machache, huku wakijua msimu uliopita waliwazidi mahasimu wao Simba na kunyakua taji la Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kufungana kwa pointi 68 ila hawakuwazidi idadi ya mabao ya kufunga.
Sango aliliambia BINGWA kuwa wao wanawasikilizia Yanga kama wako tayari kuvunja mkataba wa mchezaji huyo na klabu yake ya Prisons na dau analohitaji.
“Tumezungumza na Yanga ila kwa sasa tunawasikiliza kama watakuwa tayari kuvunja mkataba na Prisons na kutoa dau tunalohitaji (kiasi hicho kinadaiwa kuwa ni shilingi milioni 35) basi Mo Rashid atasaini,” alisema Sango.
Baada ya kumaliza mazungumzo na uongozi wa Yanga, walikubaliana kwamba atapewa mkataba wa mwaka mmoja na wakati gazeti hili linakwenda mitamboni jana usiku, mchezaji huyo alikuwa kwenye harakati za kusainishwa mkataba huo.
Mchezaji huyo ambaye alikutana na kigogo mmoja wa Yanga na kujadili masilahi yake kabla ya kusaini mkataba huo, ambapo kutwa nzima alionekana akizunguka kwenye gari ya kigogo huyo na kula bata kabla ya kuweka picha kwenye mtandao wake wa Whatsap akiwa ndani ya gari hiyo na kuiondoa muda mfupi baadaye.
- BINGWA
Tupe Maoni Yako