Mchezaji mpya wa timu ya soka ya Njombe Mji Herelimana Lewis aliyesajiliwa katika dirisha hili dogo akitokea Mukura Victory ya Rwanda amesema yupo tayari kusaidiana na wenzake na hatimaye kuiokoa timu hiyo ambayo bado haina matokeo mazuri.
Herelimana ambaye ni raia wa Burundi na anamudu vyema nafasi ya kiungo, amesema anatarajia kufanya vizuri ukizingatia toka ajiunge na wenzake ameona ni wachezaji ambao wanajituma.
-Ndo kwanza nimefika, nimeridhishwa na mazingira ya hapa, pia tunafanya mazoezi mazuri matumaini yangu ni kuwa nitasaidiana na wenzangu ili tuweze kupata matokeo mazuri, kambini safi tu’ Herelimana amesema.
Aidha mchezaji huyo ameonekana kutoridhishwa na aina ya chakula ambacho wamekuwa wakipatiwa wanavyokuwa kambini na ameshauri uongozi kuangalia namna ya kubadilisha chakula na mambo mengine madogo madogo.
-Kuna mambo madogo madogo tu ambayo ningependa uongozi uyarekebishe, wachezaji wengi tunakula chakula lakini hakijawa vizuri,” amesema.
Wachezaji wengine waliosajiliwa.
Herelimana ni miongoni mwa wachezaji wapya ambao wamesajiliwa na Njombe Mji, wengine ni Mkameruni Etienne Ngladjo kutoka Sunrise FC ya Rwanda, Mohammed Titi kutoka Singida United, Nickson Kibabage na Muhsin Malima wote kutoka Mtibwa Sugar.
Herelimana anajiunga na Njombe Mji akiwa na jukumu kubwa la kukisaidia kikosi hicho cha kocha Mlange Kabange kutoka mkiani mwa msimamo wa ligi kwani bado wapo nafasi ya 15 wakiwa na alama 8 katika michezo 11.
Mchezo wa raundi ya 12 Njombe Mji watakuwa nyumbani Disemba 30 kucheza na ‘Simba wa bonde la ufa’ Singida United kwenye uwanja wa Sabasaba uliopo mjini Njombe.
Tupe Maoni Yako