Saturday, December 9, 2017

Mawingu Tz

Bwana Weeh Kumbe Banda Na Msuva Tishio Kinoma Aisee

Wachezaji wa kimataifa wa Tanzania, beki Abdi Banda wa Baroka ya Afrika Kusini na Simon Msuva wa Difaa El Jadidi ya Morocco wameendelea kutikisa kwenye mataifa hayo kwa kuonyesha viwango vya hali ya juu.
Ni Msuva na Banda ambao wanaonekana kufanya vizuri zaidi kwa sasa, ukimuondoa Mbwana Samatta anayeuguza majeruha na Elias Maguli ambaye hakuwa na msimu mzuri na Dhofar ya Oman kabla ya kuachiwa huru.
Msuva amekuwa akitumiwa na kocha wake mkuu, Abderrahim Talib kama mshambuliaji amefanikiwa kufikisha jumla ya mabao 15 tangu ajiunge na timu hiyo Julai 28, mwaka huu.
Kabla ya kuanza kwa msimu mpya wa Ligi Kuu Morocco ‘Batola Pro’ na Kombe la Mfalme nchini humo, Msuva alifunga mabao 9 kwenye michezo 13 ya kirafiki.
Baada ya kuanza kwa msimu wa 2017/2018, Msuva ameifungia Difaa mabao 2 kwenye kombe la mfalme huku kwenye Batola Pro akifunga mabao 4 ndani ya michezo 10.
“Siri ni kujituma, niliamini kuwa naweza kufanya makubwa hata huku kama ilivyokuwa nyumbani, pamoja na Mungu kuwa ananisimamia ila pia kuwa pamoja na timu kwenye maandalizi ya msimu kumenifanya kuzoeana na wachezaji wenzangu kwa haraka.
“Tulicheza michezo 13 ya kirafiki kwa kiasi kikubwa ilinijenga kabla ya kuanza kwa msimu,cha ziada nilichokuwa nakifanyia kazi baada ya msimu kuanza ni kuzoea ligi,”alisema Msuva.
Pia, Msuva ameteuliwa kuwa kwenye kikosi bora cha Batola Pro kwa Novemba, kufuatia kiwango alichokionyesha ndani ya mwezi huo kwa kufunga mabao 2 na kutengeneza mengine 2.
“Hii ni mara yangu ya kwanza,nimejisikia furaha sana ila nimechukulia kama deni kwa kuona nadaiwa ili nifanye vizuri zaidi,” alisema Msuva.
Uwepo wa mshambuliaji huyo wa zamani wa Yanga, umechangia kwa kiasi kikubwa kuifanya Difaa kuwa kwenye nafasi ya pili ya msimamo wa ligi hiyo ikiwa na pointi 17 huku wakizidiwa na Hassania Agadir inayoongoza ligi kwa pointi 19.
Naye beki wa kati, Banda amekuwa mtu muhimu mno kwenye eneo la ulinzi la Baroka ambayo imeshushwa hivi karibuni kwenye kilele cha msimamo wa Ligi Kuu Afrika Kusini ‘PSL’ hadi nafasi ya 3 kufuatia kufungwa kwao mabao 4-0 na Mamelodi Sundowns ‘Masandawana’.
Baroka ipo kwenye nafasi hiyo kwa utofauti wa mabao ya kushinda na kufungwa, Masandawana inaongoza kwa pointi 19 ambazo ni sawa na zile za Chippa United ambao wapo nafasi ya 2.
“Ligi imekuwa ngumu sana, walioanza vibaya wameanza kurejea kwenye hali zao hivyo ni ngumu sana kupata matokeo ya ushindi mara kwa mara, tulizidiwa baadhi ya vitu ndiyo maana wametufunga ila bado tutaendelea kupigania nafasi za juu.
“Uwezekano wa kuchukua ubingwa upo ila ni mapema kwa sasa kuanza kulizungumzia hilo,” alisema Banda.
Tangu atue Baroka, Banda amekuwa mchezaji muhimu kwenye kikosi hicho ambacho amekichezea michezo yote 13 ya PSL, katika michezo hiyo ni mara 2 tu wamepoteza.
Pia, Banda ameifungia timu hiyo bao moja kwenye mchezo ambao walitoshana nguvu kwa kufungana bao 1-1 na Orlando Pirates.
Uwezo wa Banda umezivutia Kaizer Chiefs, Kaizer Chiefs na Orlando Pirates ambazo zimekuwa zikionyesha nia ya kumhitaji beki huyo wa zamani wa Simba.
“Ni kweli Januari naweza nikahama ila itafahamika baadaye kuwa nitajiunga na timu gani ila nitajiunga na timu kubwa tu,” alisema Banda.

Tupe Maoni Yako