Friday, December 29, 2017

Mawingu Tz

Alichokisema Kocha Wa Ndada Kinatisha Jamani Kuhusu Mechi Ya Kesho


KOCHA mkuu wa timu ya Ndanda FC, Malale Hamsini, ametamba kuwa wapinzani wao Simba hawatachomoka katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, utakaochezwa kesho kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona mkoani Mtwara.
Akizungumza na BINGWA kwa njia ya simu jana kutoka Mtwara, Malale alisema mwaka huu wamedhamiria kukomesha ubabe wa Simba hivyo watahakikisha hawatoki salama ndani ya dakika 90.
“Tumejipanga kushinda, haijalishi tunacheza na timu gani sisi lengo letu ni kupata pointi tatu, hivyo Simba watambue tumejipanga kukabiliana nao na tumedhamiria kushinda katika uwanja wetu wa nyumbani,” alisema.
Aliongeza kuwa mara nyingi wamekuwa wakifungwa na Simba, lakini safari hii wamejipanga kikamilifu kubakiza pointi tatu nyumbani.
Kocha huyo pia aliwamwagia sifa wachezaji watatu waliosajiliwa katika dirisha dogo ambao ni Mrisho Ngassa, Ame Ally na Salum Telela, huku akitamba kuwa nyota hao ndio watakuwa silaha za kumwangamiza mnyama Simba.
“Ngassa na Telela wapo vizuri sana, nitawatumia kama silaha katika mchezo dhidi ya Simba, Ame alichelewa kuripoti kambini hivyo sitamtumia katika mechi hiyo,” aliongeza Malale.
Akielezea kuhusu wachezaji wengine wa kikosi hicho, Malale alisema wapo fiti hivyo kazi aliyonayo ni kutafuta mbinu za kupanga kikosi bora ili waweze kutimiza malengo ya kuvuna pointi tatu muhimu dhidi ya Wekundu hao wa Msimbazi.
Aliongeza kuwa matokeo ya ushindi yatawaweka katika mazingira salama zaidi kwenye msimu wa Ligi Kuu ambapo sasa wanashika nafasi ya 11 baada ya kujikusanyia pointi 11.

Tupe Maoni Yako