Wednesday, December 6, 2017

Mawingu Tz

Tuchague Kujifunza Na Kukielewa Kinywa Cha Mo Dewji



HATIMAYE klabu ya Simba imefanikiwa kupiga hatua moja kuelekea Kaanani. Hatua moja kuelekea ilipo nchi ya ahadi. Nchi inayotiririka maziwa na asali.
Haikuwa rahisi. Ilikuwa safari ya jasho la damu. Safari ya jua na mvua, lakini mwisho wa siku wamefika na wamefanya mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji wa klabu yao.
Sasa Simba ni kampuni. Itaendeshwa kwa mfumo wa hisa na mwekezaji aliyebeba jukumu kubwa la hisa za Simba ni bilionea kijana wa Afrika, Mohammed Dewji. Mambo ya kuchangishana hela za vifusi wameshayapa kisogo.
Kumekuwa na sintofahamu nyingi katika mchakato huu. Ulianza kwa maswali na umekamilika kwa maswali. Mpaka leo tunapoitaja Simba kama Kampuni bado tuna maswali.
Mpaka leo tunapomtaja Mo Dewji kama mwekezaji wa Simba bado kuna maswali vile vile. Mo ni mmiliki wa Simba? Amechukua hisa ngapi? Kwanini Serikali inasimama kidete kila linapokuja suala la mabadiliko?
Tumechukua mfumo wa nchi gani? Simba itaendeshwa kama klabu gani? Tutegemee nini kutoka kwa Mo Dewji? Haya ni maswali yanayotembea kwenye vichwa vya wapenda soka kwa sasa.
Tuzame kusaka majibu na tuanze na kutazama jinsi klabu kubwa Ulaya zinavyoendesha mambo yao.
Sheria ya Bundesliga ikoje?
Kabla ya 1998, klabu za mpira Ujerumani zilikuwa zikimilikiwa na wanachama. Hazikuwa taasisi zinazojiendesha kwa faida na kulikuwa na sheria kali za kuzuia mtu/kampuni binafsi kuwekeza katika timu hizi.
Lakini ilipofika Oktoba 1998, Chama cha Soka Ujerumani (DFB), kilifanya marekebisho ya sheria kwa kuziruhusu klabu kuingia katika mfumo wa kujiendesha kama kampuni na kuruhusu wawekezaji.
Hata hivyo, pamoja na mabadiliko hayo, DFB waliweka kipengere cha “50+1 rule”, kilichoelekeza kuwa ni lazima asilimia 51 za umiliki wa timu ubaki kwa klabu.
Asilimia 49 za umiliki zikatolewa kwa mtu/ kampuni itakayopenda kuwekeza. Sheria hii ilikuwa na maana ya kuzuia mwekezaji kuwa na mamlaka ya moja kwa moja ya kuiendesha klabu.
Itazame Bayern Munich. Klabu inamiliki hisa asilimia 75 mpaka sasa huku asilimia 25 zilizobaki zikimilikiwa na kampuni ya vifaa vya michezo ya Adidas na kampuni ya kutengeneza magari ya Audi.
England mambo yako vipi?
Hadithi ni tofauti na Ujerumani. Mfumo wa England ni tofauti na mataifa mengine. Mtu/ kampuni ana uwezo wa kuinunua klabu na akawa na kauli ya mwisho kwenye maamuzi.
Mfano wa timu za England zinazomilikiwa na watu ni pamoja na Chelsea, iliyo chini ya Mrusi, Roman Abramovich, Newcastle (Mike Ashley), Manchester United (Familia ya Glazer) na Liverpool (John W. Henry).
Lakini pia ziko klabu ambazo zimebaki kwenye mfumo wa hisa, lakini sheria zinaruhusu mtu/ kampuni kuwa na hisa zaidi ya asilimia 50, hivyo kuwa na maamuzi ya mwisho katika kuiongoza klabu.
Mfano wa karibu wa klabu iliyo kwenye mfumo wa hisa wa aina hii ni Arsenal, ambayo Bilionea E. Stanley Kraonke, anamiliki hisa 67.5, huku Alisher Usmanov akiwa na hisa 30.4.
Klabu nyingine zilizo kwenye mfumo huu ni AFC Bournmouth, Burnley, Tottenham Hotspurs na nyingine nyingi.
Barca na Madrid kukoje?
Miongoni mwa klabu kongwe barani Ulaya zinazotumiwa sana kwenye mifano na wanachama/ mashabiki wa soka Tanzania ni Barcelona na Real Madrid.
Hizi ni klabu za wanachama. Zilikuwa hivyo na ziko hivyo mpaka leo hii. Na kitu cha kushangaza zaidi ni kuwa, klabu hizi ambazo ziko kwenye mfumo huu unaonekana ‘kinyesi’ na wengi hapa Tanzania, ndizo klabu tajiri na zenye mafanikio makubwa zaidi duniani.
Wamefanikiwaje? Hili ndio swali ambalo wengi tumesahau kujiuliza na kujifunza kutoka kwao. Tumebaki tukiwataja na kulalamika tu.
Real Madrid na Barcelona ni timu za wanachama zenye mfumo wa kipekee na tofauti kidogo na klabu zetu. Wenyewe wametengeneza kikundi cha wanachama kinachoitwa ‘socios’, ambao ndio wanaongoza klabu.
Kwa mujibu wa mkutano wa mwaka 2014, ‘socios’ ilikuwa na wanachama 91,000. Hawa ndio wenye mamlaka ya kupiga kura na kuchagua Rais na kina nani wakuingia kwenye bodi ya kuiendesha klabu yao.
Kila mwanachama wa ‘social’, hulipa kiasi cha dola milioni 140 kwa mwaka kama sehemu ya kuchangia uendeshaji wa klabu yao. Mtihani mkubwa kwa klabu za Tanzania uko katika kipengele hiki.
Tanzania tumeiga kwa Wajerumani?
Baada ya presha kubwa ya wanachama/ viongozi wa Simba kutaka kufanya mabadiliko ya kuiendesha klabu yao, huku kukiwa na taarifa kuwa Bilionea Mohammed Dewji, anataka kununua asilimia 51 za klabu hiyo kwa asilimia 49, Baraza la Michezo Tanzania (BMT), likatoa kauli.
Oktoba 27, 2017, BMT wakatengeneza sheria ya kuziongoza Klabu za Tanzania zinazotaka kufanya mabadiliko ya kiuendeshaji, kutoka kwa wanachama hadi kuwa kampuni.
Sheria hii ikaeleza kuwa mwekezaji anatakiwa kuwa na hisa zisizozidi asilimia 49, huku idadi ya hisa zilizobaki (asilimia 51), zikiachwa mikononi mwa klabu (wanachama).
Kwa jicho la kawaida kabisa ni wazi kuwa BMT waliamua kupita katika njia ambayo Chama cha Soka Ujerumani (DFB), kilipita miaka 19 iliyopita.
Faida na hasara za mfumo wa hisa tuliochagua
Kama ilivyo kwa Wajerumani, Serikali imepanga kuubakiza mpira katika asili yake. Kuubakiza mpira katika hisia za mashabiki na si kuwa mali ya mtu mmoja.
Labda kama hujanielewa hapa, turudi kwenye mfano wa Cardiff City.
Klabu hii inamilikiwa na bilionea wa Malaysia, Vincent Tan, ambaye mwaka 2012 aliamua kubadilisha rangi ya jezi kutoka Blue na kuwa nyekundu kwa sababu za kibiashara.
Tan alidai kuwa Cardiff wangeweza kuwa na soko kubwa la biashara ya jezi katika Bara la Asia kama watatumia jezi nyekundu na kuachana na rangi yao ya asili.
Lakini baada ya fujo kubwa kutoka kwa mashabiki wa klabu hiyo, bilionea huyo aliamua kurejesha rangi ya blue. Huu ni mfano mwepesi wa jinsi mtu/ kampuni ikiwa na mamlaka ya moja kwa moja katika timu za soka.
Faida nyingine ni kuipa klabu nafasi ya kufanya mabadiliko ya kiuongozi pindi watakapoona mwekezaji anakwenda tofauti na makubaliano yao.
Wakati mwingine wawekezaji huzitumia klabu kama sehemu ya mipango yao ya kibiashara na si kwa faida za kimchezo. Itazame Liverpool inavyosota na jinsi mmiliki wake anavyoiendesha klabu.
Pia mfumo huu hulinda wawekezaji kuzitia klabu kwenye madeni makubwa ambayo baadaye wakishindwa kuyalipa huzitia kwenye hasara ya kupotea kwenye ramani ya soka. Itazame Parma ilivyoteketea na madeni.
Hasara ya mfumo huu ni kunyima haki klabu zilizo na mashabiki wachache kufaidi matunda ya wawekezaji kwa maana hakuna kila mfanyabiashara atafikiria kuwekeza pesa zake kwa klabu zenye mashabiki wengi.
Tazama namna Ligi Kuu ya Ujerumani inavyokosa mvuto kwa Bayern Munich kuitawala. Haitokei kwa bahati mbaya. Wana pesa ya kutosha ya kuzidhoofisha klabu nyingine.
Hili linaweza kuikumba pia na ligi yetu kwa kupoteza mvuto kabisa kwa maana wawekezaji wote watakimbilia Yanga na Simba tu. Umeshawahi kuwaza hali ya Lipuli FC itakavyokuwa?
Kilichojificha nyuma ya pazia
Labda Serikali yetu imechungulia na kuona hatari iliyo mbele kwa kuzitoa Simba na Yanga kuwa mikononi mwa mtu mmoja. Kivipi? Tulia nikudokeze.
Simba na Yanga, ni klabu zenye mashabiki wengi kuliko vyama vya siasa, vipi kama bosi mmoja akainunua moja ya timu hizi na akaamua kuitumia kwa mtaji wa siasa? Hatavuruga amani ya nchi?
Jaribu kuitazama nguvu aliyoipata Moise Katumbi kule Congo kwa mgongo wa TP Mazembe. Kwa ustaarabu wa raia wa nchi zetu za Kiafrika, hili linaonekana kuwa tatizo kubwa kwa Serikali kutoa ruhusa hizi timu kumilikiwa na mtu mmoja.
Tunachoshindwa kuelewa kwa Mo?
Mohammed Dewji si mmliki wa Simba kama inavyoelezwa. Mo ni mwekezaji. Kama walivyowekeza Adidas kwa Bayern Munich. Kama alivyowekeza Mike Garlick pale Burnley.
Mo Dewji ameweka hisa zake Simba na kwa sheria ya Baraza la Michezo Tanzania (BMT), anakosa mamlaka ya moja kwa moja ya kufanya maamuzi ya klabu ya Simba.
Chochote atakachotaka kufanya ni lazima awasiliane na bodi ya viongozi na wamiliki wengine wenye hisa 51 zilizobakia.
Tutarajie nini kwa Simba ya Mo?
Kwanza tuwapongeze viongozi wa Simba kwa ustaarabu wao na huruma yao kwa mpira wa Tanzania kwa ujumla. Hawajaibadilisha Simba pekee, bali wameleta mabadiliko makubwa ya kimpira nchini.
Mo anaweza kuanza na hisa asilimia 49 za Simba kutuonyesha ni wapi tunakotakiwa kwenda. Soka la kuendesha kwa michango ya elfu kumi za kadi na magroup ya Whats App limeshapitwa na wakati. Mpira wa kisasa unahitaji hela.
Simba inakwenda kuwa timu kubwa Afrika kama Serikali, mashabiki na wadau wa soka nchini watamuunga mkono Mo Dewji katika harakati zake za kuukomboa mpira wa Tanzania. Ni mkombozi kweli.
-Bingwa

Tupe Maoni Yako