Monday, December 4, 2017

Mawingu Tz

Okwi Amzungumzia Chirwa

LIGI Kuu Bara imesimama kwa takribani wiki tatu kupisha michuano ya Kombe la Chalenji inayofanyika Kenya, lakini hilo halimfanyi mshambuliaji wa Simba, Emmanuel Okwi kuacha kujipanga vyema.
Okwi, ambaye amefunga mabao manane msimu huu na kuwakimbiza wapachika mabao wote wa Ligi Kuu Bara, amefunguka na kusema licha ya kuwa hafungi kwenye viwanja vya mikoani, anaamini kwamba atafanya vizuri zaidi msimu huu na wale wanaobeza watatulia tu wenyewe.
Okwi anafuatwa kwa karibu na nyota wa Yanga, Obrey Chirwa mwenye mabao sita sambamba na mchana nyavu wa Prisons, Mohammed Rashid.
“Natambua kuwa katika mbio za kuwania ufungaji bora kuna wachezaji wamezidi kusogea nilipo, lakini bado naamini kuwa nitafunga katika mechi zijazo,” alisema Okwi ambaye amewahi pia kuichezea Yanga.
“Yale maumivu niliyoyapata na kukosa mechi mbili yanakaribia kuisha.
“Jambo la msingi ni kuhakikisha Simba inapata pointi tatu katika mechi zote kwani, hilo ndilo lengo letu kuu msimu huu.
“Kama wachezaji tunaangalia mafanikio ya klabu kwanza kisha mengine yanafuata.
“Pia natamani kuwa mfungaji bora ingawa bado mapema sana kuliongelea hilo.”
Okwi pia anakiri ushindani katika kuwania tuzo hiyo msimu huu ni mkali kwelikweli.

Tupe Maoni Yako